Zikiwa zimebaki wiki chache kabla ya kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili nchini linalotarajiwa kuanza rasmi Desemba 15, 2026, vinara wa ligi kuu ya NBC, Simba SC, wameripotiwa kuandaa mkakati mzito wa kufanya maboresho ili kuendana na kasi na matakwa ya Kocha Mkuu, Steve Barker.
Barker ameweka mapendekezo ambayo anaamini kama yatatekelezwa, atakuwa na kikosi ambacho kinaweza kumaliza msimu wa ligi kuu kwa kutwaa ubingwa mapema sana na kufanya vyema zaidi kwenye ligi ya mabingwa.
Habari za ndani kutoka Msimbazi zinaeleza kuwa benchi la ufundi tayari limewasilisha ripoti kwa uongozi, ikionyesha maeneo makuu yanayohitaji maboresho ya haraka ili kulinda malengo ya timu hiyo kwenye Ligi Kuu ya NBC na michuano ya kimataifa.
Simba SC inapanga kuingia sokoni kwa nguvu kusaka wachezaji wa kimataifa katika maeneo yafuatayo:
- Mshambuliaji wa Kati (Namba 9): Hili ndilo eneo linalopewa kipaumbele cha kwanza kutokana na safu ya ushambuliaji kuwa finyu. Mpaka sasa Barker anamtegemea zaidi Elie Mpanzu aliyembadilishia majukumu kutoka eneo la winga huku Ibrahim Doumbia aliyesajiliwa kwenye dirisha lililopita akiwa hatabiriki
- Kiungo wa ushambuliaji: Kocha Barker anahitaji mchezaji mwenye uwezo wa kupiga pasi za mwisho kuongeza nguvu katika eneo hilo ambalo Clatous Chama na Neo Maema wanategemewa zaidi. Suala la umri kwa Chama linatajwa kuwa sababu ya kuhitaji kuongeza nguvu katika eneo hilo kwani ni wazi kwa wingi wa mashindano ambayo Simba inashiriki, haitakuwa rahisi kwa Chama kutoa asilimia 100 kwenye kila mchezo.
- Beki wa Kati mwenye Kasi: Licha ya uzoefu wa safu ya sasa ya ulinzi, Barker amehitaji beki mpya wa kati ambaye atakuwa na kasi kusaidiana na mabeki waliopo kwa kuzingatia mahitaji ya mechi.
- Kiungo mkabaji: Yusuph Kagoma ndiye tegemeo zaidi katika eneo hilo huku Ibrahim Jabeer akitumika kwa nyakati tofauti. Nyota huyo kutoka Nigeria alianza vyema majukumu yake mwanzoni mwa msimu lakini sasa amekuwa na vipindi tofauti vya kuingia na kutoka kwenye kikosi cha kwanza.
Doumbia bado hakieleweki
Kutokana na mpango huo wa kusajili mshambuliaji mpya wa kiwango cha juu, mustakabali wa mshambuliaji raia wa Mali, Ibrahim Doumbia, uko hatarini huku akitajwa kuwa miongoni mwa wachezaji ambao wanaweza kuondoka.
Doumbia, ambaye alitua Simba akiwa mfungaji bora nchini Mali, amekuwa na vipindi visivyotabirika hata kufikia kuwachanganya mashabiki wa timu hiyo. Licha ya kufunga mabao mawili pekee tangu atua Msimbazi, zipo mechi Doumbia amekuwa msaada mkubwa kwa Simba lakini pia zipo mechi aliingia lawamani kwa kukosa nafasi nyingi za wazi.
Ni wazi kutokana na unyeti wa nafasi yake, huenda asipate muda zaidi wa kuvumiliwa kwani Simba ilimsajili kwa kazi moja tu, kufunga mabao
Tayari tetesi zinaihusisha Simba na mshambuliaji raia wa Ivory Coast, Sede Junior Dion, anayekipiga Golden Arrows nchini Afrika Kusini.
Dion anatajwa kama mbadala sahihi kutokana na nguvu na uwezo wake wa kufunga. Jina lingine lililotajwa ikielezwa ni pendekezo la Barker mwenyewe ni mshambuliaji wa zamani wa Azam FC na Yanga, Prince Dube, ambaye kwa sasa anacheza Hardrock ya Zimbabwe.
Hata hivyo, dili la Dube huenda likawa gumu kutokana na thamani yake kubwa ya mkataba inayoweza kuigharimu klabu hiyo mabilioni ya shilingi.