Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetoa rasmi ratiba ya Uchaguzi Mkuu wa Klabu ya Simba SC utakaofanyika Januari 30, 2027, huku mchakato wa uchaguzi huo ukitarajiwa kuanza Novemba 16, 2026.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Kamati hiyo, zoezi la kuchukua na kurejesha fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya klabu hiyo litafanyika kuanzia Novemba 16 hadi 20, 2026.
Baada ya zoezi hilo, kuanzia Novemba 21 hadi 23, Kamati ya Uchaguzi itatangaza orodha ya awali ya waliochukua fomu, kabla ya kutangaza majina ya wagombea waliokidhi vigezo Novemba 27, 2026, siku ambayo pia itakuwa mwanzo wa kupokea mapingamizi.
Mapingamizi dhidi ya wagombea yatapokelewa Novemba 28 na 29, huku uchambuzi wake ukifanyika Novemba 30 hadi Desemba 1. Kamati husika itasikiliza mapingamizi hayo Desemba 2 na 3, kabla ya kufanya usaili wa wagombea Desemba 4 na 5.
Desemba 6, 2026, itakuwa siku ya kutolewa kwa maamuzi kuhusu mapingamizi, na siku inayofuata, Desemba 7, Kamati ya Uchaguzi itatangaza majina ya wagombea waliokidhi vigezo vya kuendelea na mchakato wa uchaguzi.
Awamu ya rufaa na maadili
Katika awamu ya pili ya mchakato huo, kuanzia Desemba 8 hadi 12, rufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi zitawasilishwa.
Kamati ya Rufaa itasikiliza rufaa hizo kuanzia Desemba 13 hadi 17 na kutoa maamuzi Desemba 18, 2026.
Aidha, Desemba 19, kesi zinazohusu masuala ya maadili zitawasilishwa katika Kamati ya Maadili, ambayo itaanza kuzisikiliza kuanzia Desemba 20 hadi 24, kabla ya kutoa maamuzi yake Desemba 25.
Rufaa dhidi ya maamuzi ya Kamati ya Maadili zitapokelewa kuanzia Desemba 26 hadi 30, 2026. Kamati ya Rufaa itazisikiliza kuanzia Desemba 31 hadi Januari 4, 2027, na kutoa maamuzi Januari 5.
Orodha ya mwisho na kampeni
Baada ya kukamilika kwa hatua zote za uchaguzi, Januari 6, 2027, Kamati ya Uchaguzi itatangaza orodha ya mwisho ya wagombea watakaoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Simba SC.
Kipindi cha kampeni kitaanza Januari 7 na kumalizika Januari 29, 2027, ikiwa ni siku moja kabla ya uchaguzi mkuu.
Hivyo, wanachama wa Simba SC wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi huo Januari 30, 2027, siku ambayo itakuwa kilele cha mchakato mzima wa kupata viongozi watakaoiongoza klabu hiyo katika kipindi cha miaka minne ijayo.