Beki kinda wa Simba SC, Ibrahim Nindi, ana nafasi kubwa ya kuwa mmoja wa mabeki bora wa kati nchini Tanzania kutokana na mazingira mazuri ya kujifunza aliyoyapata Msimbazi, akizungukwa na mabeki wenye uzoefu mkubwa kama Rushine De Reuck na Ismail Toure.
Nindi, ambaye ni miongoni mwa wachezaji vijana wanaotazamwa kuwa na mustakabali mzuri katika soka la Tanzania, anapaswa kutumia vizuri nafasi ya kucheza na kujifunza kutoka kwa mabeki hao ambao tayari wamejijengea heshima kutokana na uwezo na uzoefu wao.
Katika kikosi cha Simba, Nindi ana bahati ya kuwa na walimu wazuri katika eneo lake la ulinzi. Rushine De Reuck na Ismail Toure si mabeki wa kawaida, ni wachezaji wenye uzoefu mkubwa ambao wanaweza kumsaidia kijana huyo kukua katika misingi ya uchezaji wa nafasi ya beki wa kati.
BARKER ALIONA KITU KWA NINDI
Usajili wa Ibrahim Nindi ni miongoni mwa mapendekezo ya kocha mkuu wa Simba, Steve Barker, ambaye alimuona kijana huyo wakati wa michuano ya CECAFA Kagame Cup iliyofanyika Rwanda mwanzoni mwa msimu.
Barker aliona uwezo na vipaji alivyokuwa navyo Nindi na kuamua kumpa nafasi ya kujiunga na kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.
Uamuzi huo unaonyesha kuwa benchi la ufundi linaamini katika uwezo wa beki huyo na linaweza kuwa na mpango wa kumkuza ili awe sehemu muhimu ya safu ya ulinzi ya Simba kwa miaka ijayo.
Nindi ana umri mdogo, lakini kucheza katika klabu kubwa kama Simba kunampa mazingira ya kujifunza soka la ushindani wa juu, jambo ambalo linaweza kuharakisha maendeleo yake.
RUSHINE NA TOURE NI DARASA KWAKE
Kitu kizuri kwa Nindi ni kwamba ameingia katika kikosi chenye mabeki ambao anaweza kujifunza mengi kutoka kwao.
Rushine De Reuck ana uzoefu wa kucheza katika mazingira yenye ushindani mkubwa, huku Ismail Toure akiwa na sifa ya utulivu, nguvu na uwezo wa kusoma mchezo.
Kwa beki kijana kama Nindi, kujifunza namna ya kufanya maamuzi ya haraka, kupanga safu ya ulinzi, kushinda mipira ya juu, kukaba washambuliaji na kuwasiliana na wenzake ni mambo muhimu sana.
Hayo ni baadhi ya maeneo ambayo anaweza kuyafanyia kazi kwa kuwa karibu na mabeki hao katika mazoezi na mechi.
Mfano mzuri ni namna Rushine amekuwa akitengeneza mazingira mazuri ya kujifunza kwa mabeki wenzake chipukizi wa Simba. Hata Vedastus Masinde amewahi kueleza namna kucheza na Rushine kulivyomsaidia kujifunza nidhamu, ushindani na kujituma.
Hivyo, Nindi anapaswa kutumia fursa hiyo badala ya kuona uwepo wa mabeki hao kama kikwazo cha kupata nafasi ya kucheza.
Safari yake Simba imeanza rasmi pale alipopewa nafasi kwenye mchezo dhidi ya Namungo Fc. Ni kweli hakufanya vyema sana lakini bila shaka ulikuwa mwanzo mzuri kwake kwani kupitia mchezo huo atajifunza na kuboresha mchezo wake zaidi.