Wekundu wa Msimbazi, Simba SC, wameendeleza rekodi yao ya kutopoteza msimu huu baada ya kupambana kiume na kutoka nyuma na kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-2 dhidi ya Namungo FC, katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.
Ushindi huo unaifanya Simba SC kufikisha jumla ya michezo 10 mfululizo bila kupoteza wala sare, ikijichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi kwa asilimia 100 na kujizolea alama zote 30.
Mchezo huo ulianza kwa kasi huku Namungo FC wakionekana kuwapa upinzani vinara hao wa ligi kuu. Iliwachukua Simba dakika tatu tu tangu filimbi ya kuanza kwa mchezo ilipopulizwa, ambapo kiungo mshambuliaji Anicet Oura aliiandikia Simba bao la kwanza akimalizia kazi nzuri ya Elie Mpanzu.
Hata hivyo, Namungo Fc walirejea mchezoni Raymond Lulendi akiisawazishia timu yake kabla ya kupachika bao la pili kwenye dakika ya 42 na kuwapeleka Namungo Fc mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Steve Barker akifanya mabadiliko ya mbinu hasa baada ya Ibrahim Doumbia kuingia akirejesha uhai Simba ikiongeza kasi ya mashambulizi.
Baada ya mfululizo wa mashambulizi, zikiwa zimesalia dakika 11 Simba walitunukiwa mkwaju wa penati baada ya Doumbia kuangushwa ndani ya eneo la hatari ambapo beki raia wa Afrika Kusini, Rushine de Reuck, alisimama imara na kuweka mkwaju huo kambani dakika ya 79 na kuisawazishia Simba kuwa 2-2.
Wakati mashabiki wakiamini mchezo huo ungemalizika kwa sare, nyota wa mchezo huo, Anicet Oura, alirejea tena kwenye ubao akiifungia Simba bao la tatu baada ya kazi nzuri ya Elie Mpanzu kwa mara nyingine.
Oura aliondoka na tuzo ya Mchezaji Bora wa Mchezo (Man of the Match) kufuatia mchango wake mkubwa wa mabao mawili.
Kwa matokeo haya, Simba SC inazidi kujikita kileleni ikiwa na alama 30 huku ikiacha ujumbe mzito kwa wapinzani wake wakubwa kwenye mbio za ubingwa msimu huu.