Vinara wa ligi kuu ya NBC Simba SC, leo usiku watashuka katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, kuwakaribisha Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC, huku wakisaka rekodi ya kusimamisha ushindi wa 10 mfululizo msimu huu.
Simba inaingia uwanjani ikiwa na morali ya juu baada ya kushinda michezo yote tisa ya kwanza ya msimu na kujizolea alama 27, hatua inayowafanya kuongoza ligi hiyo kwa kishindo.
Hata hivyo, kibarua hakitakuwa chepesi mbele ya Namungo FC, ambao kwa sasa wanashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 15 baada ya kucheza mechi 10.
Namungo wanaonekana kupania kuvuruga karamu ya ushindi ya Wekundu wa Msimbazi, hata hivyo watahitaji kuwa bora kwelikweli mbele ya Simba inayofunga kila timu inayokuja mbele yake.
Mchezo huo unatarajiwa kuanza saa 1:00 usiku katika dimba la Uhuru, uwanja ambao hakuna timu iliyotoka salama mbele ya Simba huku baadhi ya timu zikiondoka na kapu la mabao.
Namungo Fc walikuwa wa kwanza kubebeshwa zigo la mabao na SImba kwenye uwanja huo wakipigwa mabao 6-1 idadi ambayo pia 15 de Agosto walikumbana nayo kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa.
Je leo itakuwa zamu ya Namungo?