Matola: Namungo ni wagumu, Simba yapania kuendeleza ubabe Ligi Kuu
Kocha msaidizi wa Simba SC, Selemani Matola, amesema hwapaswi kuichukulia kirahisi Namungo FC, akisema wapinzani hao ni timu imara inayoweza kutoa upinzani mkubwa katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kuchezwa kesho.
Matola amesema Namungo imekuwa ikionyesha ushindani mkubwa kila inapokutana na Simba, hali inayolazimisha kikosi chake kujiandaa kwa umakini ili kupata matokeo mazuri. Amesisitiza kuwa mchezo huo hautakuwa mwepesi na wachezaji wanapaswa kuingia uwanjani wakiwa na utayari wa kutosha.
"Maandalizi ya mchezo dhidi ya Namungo Fc yanakwenda vizuri. Tunafahamu Namungo Fc ni timu imara inayoundwa na wachezaji wazuri pamoja na mwalimu wao. Pamoja na ugumu wao sisi tumejipanga kuhakikisha tunapata alama tatu," alisema
Kwa upande wa beki Antony Mligo, amesema kikosi hicho kina dhamira ya kuendeleza mwenendo wake mzuri kwa kuhakikisha kinapata ushindi na kuendelea kukusanya pointi muhimu katika mbio za ubingwa.
Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na lengo la kuendeleza rekodi yake ya kutopoteza mchezo katika Ligi Kuu msimu huu, sambamba na kulinda nafasi yake kileleni mwa msimamo wa ligi.
Mchezo huo unatarajiwa kupigwa saa 1:00 usiku katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.