Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ali, amewataka mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi uwanjani kesho, Jumatatu, Novemba 02, 2026, kuishangilia timu yao itakapovaana na Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, kuanzia saa 1:00 usiku.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Ahmed Ali amesisitiza umuhimu wa mashabiki kuendelea kuwa bega kwa bega na timu yao kila inaposhuka dimbani, akieleza kuwa mshikamano na sapoti ya mashabiki ni sehemu muhimu ya safari ya mafanikio ya Simba.
Amesema jukumu la kila Mwanasimba ni kuhakikisha anaendelea kuiunga mkono timu katika kila mchezo, huku akiwataka mashabiki kuelekeza nguvu na mawazo yao katika kuhakikisha Simba inapata pointi tatu muhimu dhidi ya Namungo FC.
Aidha, Ahmed amekumbusha kuwa ligi inaendelea na hakuna nafasi ya kupoteza mwelekeo, hivyo kila mmoja anapaswa kuungana katika kuisukuma timu kuelekea ushindi.
"Nguvu yetu ndiyo ushindi wetu na umoja wetu ndiyo mafanikio yetu. Akili zetu tuzielekeze katika kusaka pointi tatu, kwa sababu ligi haisimami kupisha mambo yetu," amesema Ahmed Ali.
Simba itashuka uwanjani hapo kesho kusaka ushindi wa 10 mfululizo na kuendeleza rekodi yao ya ushindi wa asilimia 100 msimu huu.