Baridi bado ni kali sana kwa Wanamsimbazi pale kileleni baada ya leo kuandikisha ushindi wa tisa mfululizo wakiichapa Fountain Gate bao 1-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Manyara.
Ilikuwa ni mechi ambayo Simba ilihitaji uzoefu wake kuondoka na alama zote tatu kwa bao la Rushine de Reuck aliyekwamisha mpira kambani kwenye kipindi cha kwanza kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabu uliochongwa na Nathaniel Chilambo.
Unaweza kusema Fountain Gate leo walijipanga kucheza dhidi ya Simba ingawa pia ile kasi ya vijana wa kocha Steve Barker ni kama ilipungua.
Ni aina ya mechi ambazo alama tatu ndio matokeo muhimu zaidi kwani ushindi huo unaifanya Simba irejeshe gap la alama tano kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 27.