Mlinzi wa kulia wa Simba SC, Nathaniel Chilambo, ameendelea kuwa gumzo kubwa miongoni mwa mashabiki wa soka nchini kufuatia kiwango chake bora na uwezo mkubwa wa kubadilika kulingana na mahitaji ya timu uwanjani.
Katika mchezo wa hatua ya pili ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) uliopigwa Jumatano, Oktoba 21, 2026, Simba SC ilionyesha soka safi na kuibuka na ushindi mnono wa mabao 6-1 dhidi ya wenyeji wao, 15 de Agosto ya Equatorial Guinea, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kufuatia makubaliano ya klabu zote mbili
Licha ya wenyeji 15 de Agosto kujaribu kuzuia kwa nidhamu katika dakika za mapema, ukuta wao ulivunjwa katika dakika ya 43 pale Nathaniel Chilambo alipofunga bao la kwanza na kuwapeleka Wanasimba mapumziko wakiwa kifua mbele kwa goli 1-0.
Bao hilo liliondoa presha na kufungua milango ya mabao mengine matano katika kipindi cha pili yaliyowekwa kimiani na Elie Mpanzu (dk 56), Ibrahim Doumbia aliyefunga mawili (dk 64, 88), Keletso Makgalwa (dk 72), na Anicet Oura (dk 82).
Wenyeji walipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Alozie Uwandu katika dakika za nyongeza.
Je, Chilambo ni Beki, Kiungo, au Mshambuliaji?
Jambo linalozidi kuwapasua kichwa wachambuzi na mashabiki ni mfumo na namna Chilambo anavyocheza uwanjani.
Ingawa jina lake kwenye karatasi ya mwalimu linasomeka kama beki wa kulia, majukumu yake uwanjani yanajipambanua kama mchezaji huru (undefined player).
Timu inapopoteza mpira, Chilambo anarudi haraka kwenye mstari wa ulinzi kuzuia mashambulizi ya pembeni. Simba ikiwa na mpira, anasogea eneo la katikati na kucheza kama kiungo wa ziada (inverted fullback), akisaidia kusambaza pasi na kutengeneza nafasi.
Chilambo anao uwezo mkubwa wa kupenya kuelekeka sanduku la hatari la mpinzani, jambo lililomfanya awe katika nafasi sahihi ya kufunga goli la kuongoza dhidi ya 15 de Agosto.
Usajili wake haukuwa na mbwembwe kubwa lakini unaweza kusema miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa kwenye dirisha lililopita, yeye amekuwa na mchango mkubwa mapema ziadi kikosini pengine kuliko wenzake.