Klabu ya Simba SC inafikiria kuweka utaratibu wa kuandaa Big Screen kwa ajili ya mashabiki wake kutazama kwa pamoja mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FC 15 de Agosto de Akonibé, kufuatia changamoto ya mashabiki kutoweza kushuhudia mchezo huo uwanjani.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ali, amesema klabu hiyo inaendelea na mazungumzo na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) pamoja na FC 15 de Agosto de Akonibé, ili kutafuta namna ya kuwawezesha mashabiki wa Simba kupata nafasi ya kuishangilia timu yao uwanjani.
Ahmed amesema kukosekana kwa mashabiki kwenye mchezo huo ni pigo kwa klabu na wapenzi wake, ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika kuipa timu hamasa inapokuwa kwenye mashindano mbalimbali.
Hata hivyo, amesema klabu inatafuta njia mbadala ya kuwawezesha mashabiki kujumuika na kuitazama timu yao ikipambana katika hatua hiyo ya mashindano ya kimataifa, huku maandalizi ya kuweka Big Screen yakiwa miongoni mwa njia zinazozingatiwa.
Kupitia utaratibu huo, mashabiki watapata fursa ya kukutana sehemu moja na kufuatilia mchezo kwa pamoja, ikiwa mpango huo utatekelezwa rasmi na klabu.
Simba SC inatarajiwa kukutana na FC 15 de Agosto de Akonibe katika michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo mchezo wa kwanza umepangwa kuchezwa Oktoba 20, 2026, huku mchezo wa pili ukitarajiwa kufanyika Oktoba 25, 2026.