Kiungo Mshambuliaji wa Simba SC, Anicet Oura, ametamba kuwa timu hiyo ipo tayari kuendeleza wimbi la ushindi katika michuano ya kimataifa, akiamini matokeo mazuri iliyoyapata hivi karibuni yameongeza morali na kujiamini kwa wachezaji kuelekea pambano dhidi ya 15 de Agosto ya Equatorial Guinea.
Simba inatarajiwa kuikabili 15 de Agosto Oktoba 20, katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, huku Wekundu wa Msimbazi wakilenga kuanza kampeni yao kwa matokeo chanya.
Oura amesema ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC na ule wa mabao 2-1 dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga, umeongeza imani kwa kikosi hicho kwamba kina uwezo wa kufanya vizuri hata kinapokutana na wapinzani wa kimataifa.
Kwa mujibu wa winga huyo, matokeo hayo yamekuwa chachu ya kuimarisha umoja na ari ya kupambana ndani ya kikosi, ingawa wanatambua kuwa mchezo dhidi ya 15 de Agosto hautakuwa mwepesi.
“Kushinda mechi mfululizo, ikiwemo dabi hizo, kumetuongezea morali na kujiamini. Tunajua mchezo dhidi ya 15 de Agosto utakuwa mgumu, lakini tunaamini tutafanya vizuri,” amesema Oura.
Mbali na ubora ambao Simba imeuonyesha katika mechi zake za hivi karibuni, Oura anaamini kucheza michezo yote miwili ya hatua hiyo nchini Tanzania ni fursa muhimu kwa timu hiyo, hasa kutokana na uwezekano wa kupata sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wake.
Amesema mazingira ya nyumbani yanaweza kuwapa nguvu zaidi wachezaji, huku wakipata nafasi ya kutumia vyema uungwaji mkono wa mashabiki katika harakati za kusaka matokeo yatakayowaweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.
“Jambo lingine linalotubeba ni kwamba mechi ya kwanza na ya marudiano zitachezwa Tanzania. Hilo linatufanya tujisikie tupo nyumbani, ambako tutakuwa na sapoti kubwa ya mashabiki,” ameongeza.