Wakati Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) likiwa limeelekeza mechi mbili za ligi ya mabingwa kati ya Simba dhidi ya 15 de Agosto kuchezwa jijini Dar es salaam, klabu hiyo kutoka Guinea ya Ikweta imeomba mchezo wa mkondo wa kwanza kupigwa nchini Congo.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba Ahmed Ali amethibitisha klabu kupokea taarifa ya CAF juu ya uamuzi uliofikiwa kwa mechi zote mbili kupigwa Dar hata hivyo amekiri kuwa 15 de Agosto wameandika barua CAF wakiomba mechi ya kwanza ipigwe Congo.
Ahmed amesema wanasubiri uamuzi wa mwisho kuhusu hatma ya mchezo huo wa mkondo wa kwanza kuwania kufuzu hatua ya makundi CAFCL.
"Tuliwasiliana na wapinzani wetu 15 de Agosto tukitaka kufahamu mchezo unapigwa wapi lakini hawakujibu. Baadae tukapokea taarifa kutoka Shirikisho la soka Afrika (CAF) wakielekeza kuwa mechi zote mbili zitapigwa jijini Dar es salaam."
"Hata hivyo 15 de Agosto wameibuka tena wakitaka mechi ya mkondo wa kwanza ikachezwe Congo. Hivyo mpaka sasa hatuna uhakika wa asilimia 100 tunasubiri uthibitisho wa mwisho kutoka CAF," alisema Ahmed
CAF iliwaelekeza 15 de Agosto kutafuta uwanja unaokidhi vigezo baada ya viwanja vyote walivyowasilisha awali kukosa sifa. Baada ya ukimya wa klabu hiyo, CAF ikamua mechi zote mbili kupigwa jijini Dar es salaam.
Licha ya malalamiko ya 15 de Agosto baada ya maamuzi ya CAF, ni wazi kwa muda uliobaki kuelekea mchezo huo ni ngumu kufanya mabadiliko mengine ya uwanja.
Kwa mujibu wa ratiba mechi ya mkondo wa kwanza inapaswa kupigwa Oktoba 16/18 wakati mechi ya marudiano ikipaswa kupigwa Oktoba 21/24