Wakati Simba ikiwa kwenye kilele cha mafanikio, ikitandaza soka la kitabuni na kuwapa furaha mashabiki wake, mambo bado magumu kwa mshambuliaji Ibrahim Doumbia.
Jana Simba ilishusha kichapo cha mabao 6-1 dhidi ya Mashujaa Fc katika mchezo wa ligi kuu ya NBC uliopigwa uwanja wa Uhuru.
Huu ulikuwa mchezo ambao pengine Doumbia angeweza kufungua akaunti yake ya mabao ndani ya kikosi cha Simba lakini mambo yakawa tofauti.
Mkufunzi wa Simba Steve Barker alimpa nafasi ya kuingia kwenye kipindi cha pili na pengine atajilaumu mwenyewe kwa kushindwa kufunga bao katika mchezo huo.
Alipata nafasi tatu adimu mbili zikiwa za wazi kabisa lakini akashindwa kuzitumia.
Mashabiki wa Simba waliofurika uwanja wa Uhuru walikuwa na shauku kubwa ya kushangilia bao la Doumbia lakini haikuwezekana.
Mshambuliaji huyo ameendelea kupata sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki licha ya mwenendo wa kusuasua lakini ni wazi mwenendo wake unazidi kuweka matatani hatma yake kuelekea dirisha dogo la usajili.