Kocha mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amefichua mbinu na ujumbe uliowapa wachezaji wake nguvu ya kupindua matokeo dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC, katika Kariakoo Dabi iliyopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Simba ilipata ushindi wa mabao 2-1 baada ya kuanza mchezo ikiwa nyuma kwa bao moja, matokeo ambayo yalitokana na kuendelea kuamini uwezo wa kikosi chake na kutoyumbishwa na presha ya kufungwa mapema.
Yanga ndiyo iliyoanza kupata tabasamu dakika ya tano kupitia mshambuliaji wake Peter Shalulile, aliyefaidika na shambulizi lililoanzishwa na Maxi Nzengeli. Hata hivyo, bao hilo halikubadili imani ya Barker kwamba timu yake ilikuwa na nafasi ya kurejea na kupata matokeo mazuri.
Akizungumzia mchezo huo, Barker alisema licha ya kutoridhishwa na mwanzo wa kikosi chake, aliona Simba ikizidi kupata mwelekeo kadiri dakika zilivyokuwa zikisonga, huku ikiongeza umiliki wa mpira na kuanza kuwasukuma wapinzani wao kwenye eneo lao la ulinzi.
Kocha huyo amesema hata kabla ya kwenda mapumziko, wachezaji wake walikuwa wameonyesha dalili za kuimarika na kutengeneza nafasi zilizoweza kuwapa bao la kusawazisha. Miongoni mwa nafasi hizo ni shuti la Elie Mpanzu lililogonga mwamba.
"Wakati wa mapumziko sikufanya jambo la kubadili kabisa mfumo wa mchezo, bali niliwataka wachezaji waendelee kuamini namna yao ya kucheza, watulie wanapokuwa na mpira na wasiruhusu bao walilofungwa liwaondolee kujiamini."
"Yanga ikianza kupata wakati mgumu kukabiliana na kasi yetu, wachezaji wao walionekana kuchoka kutokana na namna tulivyowalazimisha kutumia nguvu kujilinda," alisema Barker.
Ujumbe huo ulionekana kuzaa matunda baada ya Simba kurejea kipindi cha pili ikiwa na ari kubwa ya kutafuta mabao. Dakika ya 68, kiungo Neo Maema aliirejesha timu yake mchezoni kwa kufunga bao la kusawazisha na kuwapa Wekundu wa Msimbazi msukumo wa kuendeleza mashambulizi.
Haikuchukua muda mrefu kwa Simba kukamilisha kazi hiyo. Dakika nne baada ya bao la Maema, Mpanzu alitikisa nyavu za Yanga na kuifanya Simba kuongoza kwa mabao 2-1, matokeo yaliyodumu hadi mwisho wa mchezo.
Barker amesema kabla ya bao la kusawazisha, alikuwa na matarajio kwamba timu yake ingeweza kufunga ndani ya dakika 20 hadi 25 za kipindi cha pili, akiamini bao hilo lingebadilisha mwelekeo wa mchezo na kuongeza nafasi ya kupata ushindi.
Hatimaye, imani hiyo ilitimia mapema zaidi, huku mabao mawili ya kipindi cha pili yakiipa Simba ushindi muhimu dhidi ya hasimu wake mkubwa na kupanda kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kufikisha alama 21 kutokana na ushindi wa mechi zote saba