Leo macho na masikio ya mashabiki wa Simba yataelekezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, ambapo kikosi chao kitashuka dimbani kuikabili Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakaopigwa saa 1:00 usiku.
Huu ni mchezo unaobeba hisia kubwa kwa pande zote mbili kutokana na ushindani wa kihistoria kati ya miamba hiyo ya soka nchini. Hata hivyo, kwa upande wa Simba, matumaini ya mashabiki yanaongezwa na mwenendo mzuri wa timu hiyo tangu kuanza kwa msimu huu.
Kikosi hicho kimekuwa na mwanzo wa kuvutia, kikishinda mechi zote sita za ligi kilizocheza. Zaidi ya hapo, timu hiyo ya kocha Steve Barker inaingia kwenye dabi hiyo ikiwa na rekodi ya kushinda mechi 16 mfululizo za ligi tangu msimu uliopita, jambo linaloongeza imani kwa mashabiki wake.
Chama kupewa jukumu la kuongoza jahazi
Miongoni mwa wachezaji wanaotazamiwa kubeba matumaini ya Wanasimba ni kiungo mshambuliaji Clatous Chama, ambaye amejitokeza kama mmoja wa wachezaji muhimu katika kikosi cha Barker msimu huu.
Chama amekuwa na mchango mkubwa katika eneo la ushambuliaji, akiwa kinara wa mabao kwa upande wa Simba kwenye ligi kwa kufunga mabao manne hadi sasa. Uwezo wake wa kutengeneza nafasi, kusoma mchezo na kutumia fursa anazopata unampa umuhimu mkubwa katika mpambano huo.
Mbali na mchango wake wa uwanjani, Chama ana uzoefu mkubwa wa kucheza Kariakoo Derby, jambo linaloweza kuwa msaada muhimu kwa wenzake katika mchezo wenye presha kubwa kama huu.
Leo, macho yatakuwa kwake kuhakikisha anatumia uzoefu wake kuiongoza timu ndani ya uwanja, huku akiwasaidia wenzake kubaki watulivu na wenye nidhamu ya kiuchezaji katika dakika zote za pambano.
Kwa Simba, Chama si mfungaji pekee, bali pia ni mmoja wa wachezaji wanaoweza kubadili mwelekeo wa mchezo kupitia pasi za mwisho, ubunifu na uwezo wa kufanya maamuzi muhimu katika eneo la hatari.
Gueye, Oura na Mpanzu kuongeza makali mbele
Hata hivyo, safari ya Simba kuelekea ushindi haitamtegemea Chama pekee. Safu ya ushambuliaji pia inatarajiwa kuwa na jukumu kubwa kupitia nyota wake Libasse Gueye, Anicet Oura na Elie Mpanzu.
Miongoni mwao, Gueye ni mmoja wa wachezaji ambaye pengine ndio anahofiwa zaidi na Yanga kutokana na mchango wake mkubwa katika mabao msimu huu.
Gueye amekuwa mchezaji mwenye ushawishi mkubwa kwenye mashambulizi ya Simba, akiwa ametoa asisti tano na kufunga bao moja kwenye ligi. Takwimu hizo zinaonyesha uwezo wake wa kushirikiana na wenzake pamoja na kutengeneza nafasi za kufunga.
Uwezo wake wa kutumia kasi, kupenya kwenye nafasi finyu na kuwahudumia washambuliaji wenzake unaweza kuwa silaha muhimu kwa Simba katika kujaribu kuuvuruga ulinzi wa Yanga.
Katika mchezo wa aina hii, ufanisi mbele ya lango unaweza kuamua matokeo, hivyo washambuliaji wa Simba watalazimika kutumia vizuri nafasi watakazozipata.
Katika upande wa ulinzi, Simba itahitaji kuwa makini zaidi kuhakikisha inazuia mashambulizi ya Yanga na kulinda lango lake dhidi ya washambuliaji wa wapinzani wao.
Mabeki wa kati Ismail Toure na Rushine de Reuck wanatarajiwa kuwa na jukumu muhimu katika kuimarisha safu hiyo, wakisaidiana na Nathaniel Chilambo pamoja na Anthony Mligo.
Ushirikiano kati ya mabeki hao, pamoja na mawasiliano mazuri na kipa Djibrilla Kassali, utakuwa muhimu katika kuzuia makosa yanayoweza kugharimu timu.
Hali ya Nickson Kibabage pia ni eneo linaloweza kuangaliwa, hasa kutokana na nafasi aliyokuwa nayo kabla ya kuumia. Iwapo atakuwa tayari kurejea kikosini, uwepo wake unaweza kuongeza chaguo la kocha katika safu ya ulinzi.
Kagoma na Maema watakuwa na kazi kwenye kiungo
Katika eneo la kiungo, Yusuph Kagoma na Neo Maema wanatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya mpango wa Simba, hasa katika kuunganisha safu ya ulinzi na ushambuliaji.
Kagoma atahitajika kusaidia kusawazisha mchezo, kupambana kwenye mipira ya pili na kuhakikisha Simba haipotezi udhibiti wa eneo la kati kwa urahisi.
Maema, kwa upande wake, anaweza kuwa na mchango mkubwa katika kusogeza mpira mbele na kusaidia timu kutengeneza nafasi za kushambulia.
Ushirikiano wa viungo hao na Chama utakuwa muhimu katika kuhakikisha Simba inapata njia ya kupenya kwenye safu ya ulinzi ya Yanga huku ikijilinda dhidi ya mashambulizi ya kushtukiza.
Katika dabi yenye ushindani mkubwa, timu itakayoweza kudhibiti eneo la kati na kutumia vizuri nafasi zake inaweza kupata faida muhimu katika kutafuta matokeo.
Ushindi utakuwa ujumbe kwa wapinzani
Ni wazi kuwa Kariakoo Derby ya leo haitakuwa mechi rahisi kwa Simba. Yanga nayo inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na dhamira ya kupambana na kuhakikisha inapata matokeo mazuri dhidi ya watani wake wa jadi.
Iwapo Simba itafanikiwa kupata ushindi, itakuwa imeweka alama muhimu katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC na kutuma ujumbe kwa wapinzani wake kwamba dhamira yake ya kupigania taji msimu huu ni kubwa.
Saa 1:00 usiku, macho ya Wanasimba yatakuwa pale dimba la Uhuru, wakisubiri kuona timu yao ikimaliza 'ukame' wa kukosa ushindi dhidi ya Yanga kwa takribani misimu minne kwenye ligi