Rais wa Heshima na mwekezaji wa klabu ya Simba SC, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’, ameripotiwa kuweka mezani kiasi cha Shilingi Milioni 500 kama bonasi kwa wachezaji wa timu hiyo endapo watafanikiwa kuifunga Yanga SC katika mchezo wa Ligi Kuu utakaopigwa Jumamosi, Oktoba 11, 2026.
Hatua hiyo inatajwa kuwa ni mkakati wa makusudi wa bilionea huyo ili kuongeza morali na motisha kwa wachezaji kuelekea mchezo huo wa watani wa jadi, unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini na ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati.
Mbali na motisha hiyo ya fedha, ripoti za ndani kutoka kwa klabu hiyo ya Msimbazi zinaeleza kuwa maandalizi ya kambi ya Simba yamegharamiwa kikamilifu na Mo Dewji, ikiwa ni sehemu ya maelekezo yake ya kuhakikisha timu inarejesha heshima ya dabi baada ya matokeo yasiyoridhisha katika misimu ya hivi karibuni.
Siri ya Dau Kubwa
Vyanzo vya karibu na uongozi wa Simba vinasema kuwa dau hilo limeongezwa ili kuwaongezea wachezaji ari na morali ya kupambana ndani ya dakika 90.
"Mo anataka ushindi dhidi ya Yanga Jumamosi. Milioni 500 ni kwa ajili ya kusaka pointi tatu pekee dhidi ya Yanga, na kila mchezaji anafahamu uzito wa ahadi hii," kilieleza chanzo
Msimu huu Simba imeweka malengo makubwa ya kwenye mashindano ya ndani hasa ligi kuu wakiutaka ubingwa pamoja na kufanya vyema zaidi kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika.
Kumekuwa na utaratibu wa bonasi wa timu kwenye kila mchezo lakini pia kuna bonasi ambazo Mo mwenyewe huweka mezani kwa kuzingatia uzito wa mchezo husika.