Kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Kenya na mchezaji wa timu ya taifa ya Harambee Stars, Mohammed Bajaber, amerejea nchini humo baada ya kukamilisha uhamisho wa kujiunga na Nairobi United FC.
Bajaber amejiunga na klabu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Kenya kama mchezaji huru, huku akitia saini mkataba wa miaka miwili.
Mchezaji huyo alikuwa hana klabu tangu mwezi Julai mwaka huu, baada ya kutemwa na klabu ya Tanzania, Simba SC, kwa makubaliano ya pande mbili.
Kipindi chake akiwa na Simba, kilikumbwa na changamoto kadhaa, hasa majeraha ya mara kwa mara yaliyomfanya ashindwe kupata mwendelezo wa kutosha wa kucheza na kuonyesha uwezo wake kikamilifu.
Ameikataa Gor Mahia
Uamuzi wa Bajaber kujiunga na Nairobi United umeibua mshangao katika soka la Kenya, hasa ikizingatiwa kuwa kulikuwa na klabu kubwa zilizokuwa zikihitaji huduma yake.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Kenya, Bajaber alikataa ofa nzuri kutoka kwa Gor Mahia FC, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Kenya (FKFPL), ambao walikuwa wakifanya juhudi kubwa kuhakikisha wanapata saini ya kiungo huyo.
Badala yake, nyota huyo ameamua kujiunga na Nairobi United, hatua inayotajwa kuwa ni ishara ya imani yake kwa mradi wa klabu hiyo.
Kurejea kwa Bajaber nchini Kenya kunatarajiwa kuwa nyongeza kubwa kwa Nairobi United, ambayo ina azma ya kupanda daraja na kucheza Ligi Kuu ya Kenya msimu ujao.
Uzoefu wake wa kucheza katika mazingira ya ushindani, pamoja na majukumu yake katika timu ya taifa ya Kenya, unatarajiwa kuifanya Nairobi United kuwa na nguvu zaidi katika mbio za kupanda daraja.