Baada ya takribani siku 10 za maandalizi nchini Afrika Kusini, kikosi cha Simba SC kilirejea nchini mwanzoni mwa wiki na kuingia kambini kwa ajili ya mchezo unaosubiriwa kwa hamu wa dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga SC.
Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana Jumamosi, Oktoba 10, katika Uwanja wa Uhuru, huku kila upande ukiingia kwenye mchezo huo ukiwa na sababu kubwa ya kutaka kupata matokeo mazuri.
Lakini kabla ya mpambano huo, jina moja limekuwa likitawala zaidi kwenye mijadala mitandaoni, Libasse Gueye.
Mara baada ya Simba kurejea kutoka Afrika Kusini, kulienea taarifa kwamba kiungo mshambuliaji huyo raia wa Senegal amepata jeraha la kifundo cha mguu ambalo lingemuweka nje ya uwanja kwa takribani wiki nne.
Hata hivyo, taarifa hizo zilikuwa sio za kweli. Uongozi wa Simba ulithibitisha kwamba Gueye hana tatizo hilo na kwamba yupo fiti kwa asilimia 100, huku akiendelea na maandalizi pamoja na wenzake kuelekea mchezo dhidi ya Yanga.
Sasa ni hivi; Kama kuna mchezaji ambaye huenda benchi la Yanga lingetamani asionekane kwenye kikosi cha Simba Jumamosi, basi ni Gueye. Sababu ni moja kubwa, amekuwa na msimu wenye kiwango cha juu sana mpaka sasa.
Gueye ni mtambo wa mabao wa Simba
Msimu huu Gueye ameonekana kuwa mchezaji tofauti. Ameimarika zaidi, amekuwa na ushawishi mkubwa katika safu ya ushambuliaji na zaidi ya yote, amekuwa akithibitisha kwa vitendo kwa nini ni mchezaji ambaye timu pinzani haitamani kumpa nafasi.
Takwimu zinaeleza kila kitu.
Katika mabao 11 ambayo Simba imefunga kwenye Ligi Kuu msimu huu, sita yamepita kwenye mguu wa Gueye.
Hiyo ni zaidi ya nusu ya mabao yote ambayo Simba imefunga kwenye ligi.
Kwa maana nyingine, unapozungumzia uwezo wa Simba kuzalisha mabao msimu huu, huwezi kuacha kulitaja jina la Gueye.
Ni mtambo wa mabao wa Simba.
Uwepo wake kwenye Champions League ulitoa majibu
Umuhimu wa Gueye ulionekana pia kwenye kampeni za Simba katika hatua za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kiungo huyo alikosa mchezo wa kwanza dhidi ya Mighty Wanderers, ambao Simba ilifanikiwa kushinda kwa bao 1-0 ugenini.
Lakini aliporejea kwenye mchezo wa pili jijini Dar es Salaam, alitoa jibu la moja kwa moja kuhusu thamani yake ndani ya kikosi.
Gueye alifunga mabao mawili katika ushindi mkubwa wa Simba wa 6-1.
Ilikuwa ni mechi iliyodhihirisha kwamba uwepo wake unaweza kubadilisha kabisa sura ya mashambulizi ya Simba.
Amehusika mabao nane msimu huu
Licha ya msimu kuwa bado katika hatua zake za mwanzo, Gueye tayari amehusika moja kwa moja kwenye mabao manane katika mashindano yote.
Takwimu hiyo inampa nafasi ya kuwa mmoja wa wachezaji wenye ushawishi mkubwa zaidi katika soka la Tanzania kwa sasa.
Jumamosi inaweza kuwa fursa nyingine kwake kuthibitisha kile ambacho amekuwa akikifanya tangu mwanzo wa msimu.
Ni wazi, dabi ya Kariakoo ndio kipimo kikubwa ambacho anakwenda kukutana nacho pengine kuliko mechi zilizopita. Wanasimba wanasubiri kuona akiendeleza moto wake.