Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema ujio wa kocha Steve Barker umeongeza kiwango cha kujiamini ndani ya kikosi hicho, huku akisisitiza kuwa Simba haijioni kama timu dhaifu kuelekea Kariakoo Derby dhidi ya Yanga.
Ahmed amesema Barker tangu alipowasili Msimbazi hajawahi kuiona Simba kama timu inayopaswa kuwa mnyonge mbele ya mpinzani yeyote, akieleza kuwa kocha huyo ana kile alichokiita “kiburi cha kujiamini.”
Kwa mujibu wa Ahmed, hali hiyo ni sehemu ya falsafa ya Barker katika ushindani. Amesema kocha huyo alionyesha tabia hiyo hata alipokuwa akiifundisha Stellenbosch FC ya Afrika Kusini, ambako alikuwa tayari kushindana kwa ujasiri dhidi ya Mamelodi Sundowns, moja ya klabu kubwa na zenye mafanikio barani Afrika.
Mbali na kujiamini huko, Ahmed amesema Simba anaendelea na maandalizi yake kambini wakiwa na mkakati wa kushindamchezo huo.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, kutokana na rekodi za timu hizo mwanzoni mwa msimu. Simba na Yanga zote zimefanikiwa kushinda michezo sita ya kwanza ya Ligi Kuu, jambo linaloongeza hamasa kuelekea pambano hilo la watani wa jadi.
Baada ya kutofanya vyema dhidi ya Yanga katika mechi za ligi kuu kwa takribani misimu mitatu, msimu huu Wekundu wa Msimbazi wamepania kurejesha ufalme wao dhidi ya wapinzani wao wakuu na muhimu zaidi malengo ni kutwaa ubingwa wa ligi kuu walioukosa kwa misimu mitano mfululizo.