Wanasimba wekeni alama kwenye kalenda zenu! Oktoba 10, 2026, Uwanja wa Uhuru maarufu kama ‘Shamba la Bibi’ utageuka kuwa uwanja wa vita vya soka, wakati Simba na Yanga zitakapokutana katika Kariakoo Derby ya Ligi Kuu ya NBC.
Mchezo huo unaokuja ukiwa na sura mpya kutokana na matumizi ya teknolojia ya FVS pamoja na utaratibu wa viti vya namba, unatarajiwa kuanza saa moja kamili usiku, huku Simba ikiwa mwenyeji wa pambano hilo.
Lakini kabla mpira haujachezwa na kabla ya kizazi cha sasa kuanza kuandika ukurasa mwingine wa historia, kuna jina moja ambalo bado limeshikilia historia ya dhahabu ya Kariakoo Derby.
Ni jina la nguli wa Simba, Abdallah “King” Kibadeni.
Miaka inapita, vizazi vinabadilika, wachezaji wapya wanaingia na kutoka, lakini rekodi iliyowekwa na Mzee Kibadeni katika moja ya Derby kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini bado haijafutika.
Kibadeni na usiku wa kihistoria
Ni mwaka 1977.
Kariakoo ilikuwa inawaka, Simba na Yanga zilikutana katika moja ya mapambano yaliyokuja kuacha alama kubwa katika historia ya soka la Tanzania.
Lakini siku hiyo haikuwa siku ya kawaida.
Ilikuwa siku ambayo Mnyama alinguruma kwa nguvu na kuwaacha watani zao wakiwa hawana majibu.
Simba iliibuka na ushindi mnono wa mabao 6-0, matokeo ambayo hadi leo yanatajwa miongoni mwa vipigo vikubwa zaidi katika historia ya Kariakoo Derby.
Na katikati ya sherehe hiyo ya mabao, kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa na nafasi ya kipekee zaidi.
Abdallah “King” Kibadeni.
Nguli huyo alifunga mabao matatu katika mchezo huo na kuweka historia ambayo bado haijavunjwa kuwa mchezaji aliyefunga hat-trick katika Kariakoo Derby.
Kibadeni alifunga mara tatu, huku Jumanne Masimenti akiongeza mabao mawili na Selemani Sanga akifunga bao la kujifunga, na kufanya ubao wa matokeo kusomeka Simba 6-0 Yanga.
Hiyo ndiyo sababu kila Kariakoo Derby inapokaribia, jina la Kibadeni hurudi mezani.
Si kwa sababu tu ya kuwa sehemu ya kizazi cha dhahabu cha Simba, bali kwa sababu aliweka alama ambayo mpaka leo haijafutika.
Miaka inapita, rekodi bado ipo
Katika soka, rekodi zipo ili zivunjwe.
Lakini baadhi ya rekodi huishi kwa muda mrefu kiasi kwamba zinageuka kuwa sehemu ya utamaduni wa mchezo wenyewe.
Hat-trick ya Kibadeni ni miongoni mwa rekodi hizo.
Kariakoo Derby imepitia vizazi vingi. Imeona mashujaa wa aina mbalimbali, imezalisha wafungaji waliotikisa nyavu na imeshuhudia matokeo yaliyowafanya mashabiki wa pande zote mbili kuzungumza kwa miaka.
Lakini hadi sasa, hakuna aliyefanikiwa kufanya kile alichokifanya Kibadeni mwaka 1977 kufunga mabao matatu katika mchezo mmoja wa dabi hii.
Ndiyo maana jina lake bado lina uzito mkubwa kila Simba na Yanga zinapokutana.
Kutoka Kibadeni hadi kizazi cha Okwi
Kama ushindi wa 6-0 wa mwaka 1977 ulikuwa sehemu ya dhahabu ya historia ya Simba, kizazi cha baadaye nacho kiliandika ukurasa wake.
Mwaka 2012, Simba iliwakabili Yanga ikiwa na kikosi kilichokuwa na nyota kama Emmanuel Okwi na Patrick Mafisango, na mwisho wa dakika 90 ubao wa matokeo ukasomeka Simba 5-0 Yanga.
Ilikuwa ni moja ya siku ambazo mashabiki wa Simba waliishi kwa muda mrefu, huku Okwi na wenzake wakifanya Kariakoo Derby kuwa jukwaa la kuonyesha uwezo wao.
Miaka ilibadilika, wachezaji wakabadilika, lakini ujumbe ukabaki uleule: katika dabi, historia inaweza kuandikwa ndani ya dakika 90.
Kishindo kingine mwaka 2020
Mwaka 2020, Simba iliandika tena ukurasa mwingine katika historia ya kukutana na Yanga.
Katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-1, katika mchezo ambao uliwakutanisha watani hao katika mazingira yenye presha kubwa.
Mabao ya Clatous Chama, Mzamiru Yassin, Gerson Fraga na Luis Miquissone yaliipa Simba ushindi huo na tiketi ya kuelekea fainali.
Ushindi huo ukaongeza kwenye orodha ya kumbukumbu ambazo mashabiki wa Simba hupenda kuzikumbuka kila Derby inapokaribia.
Oktoba 10, ukurasa mpya unaandikwa
Sasa macho yanaelekezwa Oktoba 10, 2026.
Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa mwenyeji, huku morali ya timu ikiwa juu kutokana na mwanzo mzuri wa msimu na hamu ya kuendeleza ushindani dhidi ya watani wao.
Lakini pamoja na kelele zote za sasa, historia inabaki kuwa historia.
Na ndani ya historia hiyo, Mzee Abdallah “King” Kibadeni bado ana nafasi yake ya kipekee.
Miaka 49 imepita tangu alipofunga hat-trick yake kwenye ushindi wa 6-0, lakini hakuna mchezaji mwingine aliyefanikiwa kurudia tukio hilo katika Kariakoo Derby.
Hilo ndilo taji la dhahabu analolishikilia mpaka leo.