Wakati Simba na Yanga zikijiandaa kukutana katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakaochezwa Oktoba 10, TFF imeweka utaratibu mpya utakaohusisha matumizi ya teknolojia katika kudhibiti matukio yatakayojitokeza ndani ya mchezo huo.
Moja ya mambo mapya yatakayoshuhudiwa katika Derby hiyo ya Kariakoo ni matumizi ya mfumo wa FIFA Video Support (FVS), ambao utawapa makocha wa timu hizo nafasi ya kuomba mwamuzi apitie upya matukio fulani yanayotokea uwanjani.
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Cornel Barnabas, amesema kila benchi litapewa kadi mbili maalum kwa ajili ya kuomba huduma hiyo pale linapoona kuna tukio linalohitaji kupitiwa.
Kwa mujibu wa Cornel, jumla ya kadi nne zitatumika katika mchezo huo, huku kila benchi likiwa na kadi mbili. Hata hivyo, matumizi yake yatakuwa na muda maalum.
“Kwenye mechi kutakuwa na kadi nne za kuomba FVS itumike. Kila benchi litapewa hizi kadi mbili. Linapotokea tukio ambalo benchi linahitaji msaada wa FVS ili haki itendeke, litaonyesha kadi juu na refa ataenda kwenye FVS. Sharti ni kwamba benchi linatakiwa kuonyesha kadi yao juu ndani ya sekunde 60, haitakiwi kuchelewa hadi tukio lipite,” alisema.
Mfumo hautakuwa kwa Kariakoo Derby pekee
Cornel amesema matumizi ya FVS hayatakuwa maalum kwa mchezo wa Simba na Yanga pekee, bali ni sehemu ya mfumo utakaotumika katika michezo mingine ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hatua hiyo inalenga kuongeza matumizi ya teknolojia katika uamuzi wa matukio ya mchezo na kuwapa benchi la ufundi nafasi ya kuomba mapitio pale linapoona kuna sababu ya kufanya hivyo.
TFF yashughulikia pia usalama wa vyumba
Mbali na suala la FVS, maandalizi ya Kariakoo Derby yamehusisha pia hatua za ziada katika kuhakikisha usalama wa maeneo ya ndani ya uwanja, hususan vyumba vya kubadilishia nguo.
Cornel amesema TPLB imeandaa matumizi ya kifaa maalum cha kugundua harufu ambacho kitatumika kukagua vyumba hivyo kabla ya timu kuvitumia.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kuwepo kwa malalamiko na hofu zinazohusishwa na usalama wa vyumba vya kubadilishia nguo katika baadhi ya michezo iliyopita..
Cornel amesema kifaa hicho hakitakuwa kwa matumizi ya Kariakoo Derby pekee, bali kitaendelea kutumika katika michezo mingine ya Ligi Kuu Tanzania Bara.