Nyasi za Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam, leo zinatarajiwa kuwaka moto pale miamba miwili ya soka la wanawake nchini, Simba Queens na JKT Queens, itakaposhuka dimbani kusaka taji la Ngao ya Jamii.
Mchezo huo wa fainali unaosubiriwa kwa hamu kubwa unatarajiwa kuanza majira ya saa 10:00 jioni, ukizikutanisha timu mbili zenye mkali na historia kubwa kwenye soka la wanawake Tanzania.
Simba Queens waliingia hatua hiyo kwa kishindo baada ya kuwagaragaza mahasimu wao wa jadi, Yanga Princess, kwa mabao 3-0 katika mchezo wa nusu fainali.
Kwa upande wao, watetezi wa taji hilo, JKT Queens, walitinga fainali kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa Queens ya Kigoma.
Vita ya Vikombe na Kisasi
Fainali ya leo si tu inatafuta bingwa wa mwaka huu, bali pia inabeba taswira ya ushindani wa kihistoria tangu kuanzishwa kwa michuano hii mwaka 2023.
Simba Queens walikuwa mabingwa wa kwanza wa Ngao ya Jamii mwaka 2023, lakini JKT Queens walipindua meza na kutwaa taji hilo mara mbili mfululizo (mwaka 2024 na 2025). Simba Queens wanaingia uwanjani wakitaka kusawazisha hesabu na kurudisha heshima yao, huku JKT Queens wakipambana kulinda ufalme wao ili kubaki na kikombe hicho.
Makocha wa timu zote mbili wametamba kuwa vikosi vyao viko fiti na wachezaji wao wana morali ya juu ya kuondoka na ushindi leo jioni.
Kwa Simba Queens leo wanahitaji ushindi ili kuhakikisha wanaanza vyema msimu wakilenga kutetea ubingwa wa ligi kuu ya Wanawake waliotwaa msimu uliopita.
Kabla ya miamba hiyo kushuka dimbani, mchezo wa kusaka mshindi wa tatu utakaopigwa saa 7:00 mchana kwenye uwanja huo huo, ukizikutanisha Yanga Princess na Mashujaa Queens.