Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, ameweka wazi kuwa kambi ya timu hiyo nchini Afrika Kusini imekwenda kwa mujibu wa matarajio yake, licha ya changamoto ya baadhi ya wachezaji kuchelewa kuungana na wenzao.
Simba ipo Polokwane kwa ajili ya kipindi maalumu cha maandalizi kinacholenga kuendelea kujenga timu kuelekea michezo muhimu inayosubiriwa baada ya kurejea Tanzania.
Barker amebainisha kuwa sehemu kubwa ya kikosi tayari ina uelewa wa mfumo na falsafa yake ya uchezaji. Hivyo, kuwasili kwa wachezaji kwa nyakati tofauti hakukulazimisha benchi la ufundi kuanza upya mchakato wa maandalizi.
Kocha huyo anaonekana kutumia kambi hiyo zaidi kama nafasi ya kuendeleza kazi iliyokuwa tayari imeanza, badala ya kuichukulia kama mwanzo mpya wa msimu.
Siku za mwisho zawa muhimu
Wakati kambi ikielekea ukingoni, Simba imeendelea kukamilisha muunganiko wa kikosi chake baada ya wachezaji mbalimbali kuwasili kwa nyakati tofauti.
Miongoni mwa waliojiunga na timu katika hatua za mwisho ni Alain Anicet Oura na Ibrahim Doumbia. Wawili hao wamepata nafasi ya kufanya kazi na wenzao katika siku za mwisho za kambi, jambo ambalo Barker anaona linaweza kuwasaidia kuendana na mahitaji ya timu.
Kwa mtazamo wa benchi la ufundi, muda huo hauwezi kuonekana kuwa mrefu, lakini unaweza kutumika kuwapitisha wachezaji hao katika maelekezo muhimu ya kiufundi na namna timu inavyotaka kucheza.
Simba ilielekea Afrika Kusini ikiwa na agenda kubwa zaidi ya kufanya mazoezi ya kawaida. Kambi hiyo imekuwa sehemu ya maandalizi ya timu kuelekea ratiba yenye ushindani, ikiwemo mchezo wa Kariakoo Derby dhidi ya Yanga unaotarajiwa Oktoba 10, 2026.