Kocha Mkuu wa Simba Queens Mussa Mgosi amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa nusu fainali Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga Princess utakaopigwa kesho Jumatano kwenye uwanja wa KMC Complex.
Akizungumza kwenye mkutano na wanahabari kuelekea mchezo huo, Mgosi alisema malengo yake ni kutwaa Ngao ya Jamii hivyo wanauchukulia mchezo huo kwa umuhimu mkubwa.
"Maandalizi yetu yamekwenda vizuri, Simba Queens tunahitaji kuwa mabingwa wa michuano hii."
"Ili kutimiza mipango yetu tunahitaji kuwa bora na kuweza kupata ushindi dhidi ya mpinzani wetu."
"Tunataka kurudisha heshima yetu pamoja na kuanza vyema msimu wa ligi kuu ya Wanawake 2026/27," alisema Mgosi
Mchezo dhidi ya Yanga Princess utapigwa uwanja wa KMC Complex saa 12 jioni ukitanguliwa na mchezo wa kwanza wa nusu fainali kati ya JKT Queens dhidi ya Mashujaa Queens.