Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, amesema kambi ya timu hiyo iliyowekwa mjini Polokwane, Afrika Kusini, imekuwa na mazingira bora yanayokidhi viwango vya kimataifa na kuwapa wachezaji kila wanachohitaji katika maandalizi yao.
Barker amesema ubora wa mazingira na viwanja wanavyotumia umewezesha timu kufanya mazoezi kwa utulivu na kuzingatia maeneo muhimu ya maandalizi ya msimu.
“Viwanja vyao viko kwenye ubora wa Kimataifa, tunapata kila kitu tunachohitaji humu ndani.”
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini amesema Simba ilihitaji kambi ya aina hiyo kutokana na kutokuwa na maandalizi kamili ya msimu (pre-season), hivyo muda waliopo Polokwane unalenga zaidi kuwaongezea utimamu wa miili wachezaji na kuboresha maeneo mbalimbali ya kiufundi.
“Tulihitaji mazingira ya aina hii kwani kumbuka hatukuwa na pre-season iliyokamilika. Hivyo tulihitaji mazingira ya aina hii ili kuimarisha utimamu wa miili ya wachezaji na kuboresha maeneo muhimu,” alisema Barker.
Barker ampongeza Mo Dewji
Barker pia amempongeza Rais wa Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’, kwa kuwezesha mazingira hayo ya maandalizi, akisema kambi hiyo inaweza kuwasaidia kuongeza kile ambacho timu ilikikosa mwanzoni mwa msimu.
Kwa mujibu wa kocha huyo, mazingira mazuri ya mazoezi ni sehemu muhimu katika kuhakikisha wachezaji wanaendelea kujenga utimamu wa mwili na kujiandaa vyema kwa changamoto zinazowakabili.
Simba siku ya nne kambini
Simba imeweka kambi ya siku 10 mjini Polokwane, Afrika Kusini, kwa ajili ya kujiandaa na michezo ijayo.
Leo, Wekundu wa Msimbazi wameingia siku ya nne tangu kuanza kwa kambi hiyo, huku benchi la ufundi likitumia muda huo kuendelea kuimarisha utimamu wa wachezaji pamoja na maeneo mbalimbali ya kiufundi.