Mshambuliaji wa Simba SC, Ismail Mgunda, ameonyesha kujiamini kuelekea Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga SC, akisema anaamini kwa asilimia 100 kuwa Wekundu wa Msimbazi wana uwezo wa kuibuka na ushindi katika mchezo huo.
Mgunda, ambaye amejiunga na Simba akitokea Mashujaa FC, anajiandaa kucheza Dabi yake ya kwanza ya Kariakoo tangu kuwasili Msimbazi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu wa 2026/27.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Mgunda amesema kile anachokiona katika mazoezi pamoja na maandalizi waliyofanya katika kambi ya Afrika Kusini kimemjengea matumaini makubwa kuhusu uwezo wa kikosi hicho.
“Ninaamini kwa asilimia 100 kwamba tunaweza kupata ushindi kwenye Dabi ya Kariakoo. Kile ambacho nimekiona kwenye mazoezi na maandalizi yetu kinanipa matumaini makubwa,” alisema Mgunda.
Mshambuliaji huyo amesema maandalizi waliyoyafanya yamewapa utayari wa kukabiliana na mchezo huo, huku kila mchezaji akitambua ukubwa na umuhimu wa Dabi hiyo kwa klabu na mashabiki wake.
“Tunajiandaa vizuri, hasa kupitia kambi yetu hapa. Kila mchezaji anaelewa umuhimu wa mchezo huu na tuko tayari kupambana kwa ajili ya timu,” alisema.
Kwa Mgunda, mchezo huo utakuwa wa kipekee pia kutokana na kuwa Dabi yake ya kwanza ya Kariakoo akiwa mchezaji wa Simba. Amesema anafahamu ukubwa wa mchezo huo na yuko tayari kutoa mchango wake kuhakikisha timu inapata matokeo inayoyahitaji.
“Hii itakuwa Dabi yangu ya kwanza tangu nijiunge na Simba, hivyo ninaiona kama mechi kubwa na yenye umuhimu wa kipekee kwangu. Nitatoa kila kitu kuhakikisha timu inapata matokeo tunayoyataka"
“Tunawaheshimu Yanga kama wapinzani wetu, lakini tunachoangalia ni maandalizi yetu na namna tutakavyocheza. Nina imani kubwa na kikosi chetu,” alisema.
Simba imeweka kambi ya siku 10 Afrika Kusini kujiandaa na mchezo huo utakaopigwa Oktoba 10 pamoja na mechi nyingine za ligi kuu na ligi ya mabingwa (CAFCL).