Kocha wa Simba, Steve Barker, amefichua sababu iliyo nyuma ya kiwango bora cha beki wa kati Rushine De Reuck, akisema mwendelezo wa kucheza umemsaidia kurejesha ubora aliokuwa nao kabla ya kukumbwa na majeraha.
Barker amesema De Reuck amekuwa na mchango mkubwa katika kikosi cha Simba tangu alipowasili Msimbazi, huku akisisitiza kuwa alikuwa tayari anaufahamu uwezo wa beki huyo tangu miaka ya nyuma alipokuwa akiichezea Maritzburg United nchini Afrika Kusini.
“Rushine amekuwa vizuri kwa Simba tangu nilipowasili. Nilijua ubora wake miaka mingi iliyopita hata alipokuwa Maritzburg ambako alifanya vizuri kabla ya kuhamia Sundowns,” alisema Barker.
Barker amebainisha kuwa De Reuck ameongeza utulivu na ubora katika safu ya ulinzi ya Simba, huku uwezo wake wa kucheza na mpira na kuanzisha mashambulizi kutoka nyuma ukiwa miongoni mwa vitu vinavyomtofautisha.
Kocha huyo amesema mwendelezo wa kucheza umemsaidia De Reuck kurejesha kiwango chake, akieleza kuwa huenda hiki kikawa kipindi kirefu zaidi ambacho beki huyo amepata nafasi ya kucheza kwa mwendelezo katika maisha yake ya soka.
“Anachofanya kwa Simba, kwa upande wa utulivu na ubora anaouleta kwenye ulinzi na hata kwenye kushambulia ni kitu kizuri sana. Ana utulivu akiwa na mpira na anaweza kuanzisha mchezo kutoka nyuma hata katika mazingira magumu,” alisema Barker.
De Reuck muhimu katika mwanzo wa msimu
Kiwango kizuri cha De Reuck kimeendelea kuonekana katika msimu huu, ambapo amekuwa sehemu ya kikosi cha Simba kilichoanza kampeni ya Ligi Kuu kwa ushindi wa mechi sita mfululizo.
Matokeo hayo yameifanya Simba kufikisha pointi 18, sawa na Yanga, ambao wanaongoza msimamo wa ligi.
Rushne ni sehemu ya kikosi cha Simba kilichoweka kambi Afrika Kusini ambako wanaendelea na maandalizi wakti ambao ligi zimesimama kupisha kalenda ya FIFA.
Kambi hiyo ni sehemu ya maandalizi ya ratiba yenye msongamano inayowakabili Wanasimba, ikiwemo Kariakoo Dabi dhidi ya Yanga Oktoba 10 pamoja na michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.