Baada ya kuwasili mji wa Polokwane hapo jana, kikosi cha Simba leo kimeanza maandalizi yake ya siku 10 kujiandaa na mikiki mikiki ya ligi kuu na ligi ya mabingwa itakayoendelea baada ya mapumziko ya kalenda ya FIFA.
Kocha Mkuu wa Simba Steve Barker sambamba na baadhi ya mastaa kama Neo Maema, Keletso Makgalwa, Rushine de Reuck na Ibrahim Jabeer walioungana na timu Afrika Kusini, wameshiriki mazoezi hayo ya kwanza.
Nyota wengine hasa wale wa kigeni ambao walisafiri kwenda makwao kwa ajili ya mapumziko ya siku chache, wanatarajiwa kuungana na kikosi hapo Polokwane.
Simba itakuwa na siku 10 za moto kukamilisha maandalizi yake kabla ya kurejea Dar es salaam kuwakabili watani zao Yanga kwenye mchezo wa ligi kuu raundi ya 7.
Mtanange huo utakaopigwa Oktoba 10, huenda ukachezwa kwenye uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, uwanja ambao Simba inacheza mechi zake za nyumbani ligi kuu ya NBC msimu huu.