Wakati Ligi Kuu ya NBC ikisimama kwa takribani wiki tatu kupisha kalenda ya FIFA, Simba SC imeamua kutumia kipindi hicho kujiweka tayari zaidi kwa ajili ya kuendeleza kasi yake ya ushindi msimu huu.
Wekundu wa Msimbazi wameelekea Afrika Kusini kuweka kambi ya siku 10, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kikosi hicho kabla ya kurejea kwenye mashindano na kukutana na wapinzani wao wakubwa, Yanga, katika Derby ya Kariakoo itakayochezwa Oktoba 10.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kambi hiyo imelenga zaidi kuhakikisha kikosi kinaendelea kuwa katika hali ya ushindani licha ya ligi kusimama.
Akizungumza muda mfupi kabla ya kikosi hicho kuondoka jijini Dar es Salaam, Ahmed alisema mapumziko ya kalenda ya FIFA hayatazuia Simba kuendelea kujinoa, badala yake yametumiwa kama fursa ya kukiandaa zaidi kikosi.
"Kambi yetu ya siku 10 inalenga kuwaweka wachezaji katika utimamu mzuri wa mwili na kuhakikisha kiwango cha timu hakishuki kutokana na kusimama kwa ligi."
“Tunamshukuru na kumpongeza Rais wa Simba SC na mwekezaji, Mohammed Dewji kwa kujitoa kwake kugharamia kambi hii,” alisema Ahmed
Simba imeanza msimu kwa kasi, ikiwa imeshinda mechi zote nane ilizocheza katika mashindano yote hadi sasa.
Zaidi ya hilo, Wekundu wa Msimbazi wameweka rekodi ya kushinda mechi 16 mfululizo za Ligi Kuu, ikiwa ni mwendelezo wa kasi waliyoimalizia msimu uliopita.
Kambi hiyo ya Afrika Kusini, iliyogharamiwa na Rais wa Heshima wa Simba, bilionea Mohamed Dewji ‘Mo Dewji’, imekuja wakati ambao benchi la ufundi lina jukumu la kuhakikisha kasi hiyo haikatiki.