Rushine afunguka maisha yake Simba 'Nilikuja nikiwa na hofu kubwa'

Mwana Msimbazi By Mwana Msimbazi
β€’
23 Sep 2026
Rushine afunguka maisha yake Simba 'Nilikuja nikiwa na hofu kubwa'

Beki wa kati wa kimataifa wa klabu ya Simba SC, Rushine De Reuck, amefunguka kwa kina kuhusu safari yake ya soka, hofu kubwa aliyokuwa nayo kabla ya kutua nchini, na sababu zilizomfanya aondoke katika miamba ya soka ya Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Fatema Dewji kwenye kipindi cha Micro Moments of Self-Love, De Reuck ameweka wazi kuwa uamuzi wa kuja Tanzania haukuwa mwepesi kutokana na changamoto za kisaikolojia alizokuwa akizipitia.

Hofu na Kujitilia Shaka

Beki huyo alikiri kwamba kukosa nafasi ya kucheza kwa muda mrefu akiwa Afrika Kusini kulishusha viwango vyake vya kujiamini, jambo lililomfanya aingiwe na uoga alipopata fursa ya kujiunga na Simba.

"Nilikuja hapa nikiwa na hofu kubwa sana. Nilikuwa nimekaa nje kwa muda mrefu bila kucheza kule Afrika Kusini, na nilianza hata kujitilia shaka kama bado nina uwezo wa kucheza soka la ushindani," alisema De Reuck.

Aliongeza kuwa mtu pekee aliyemfahamu kabla ya kutua nchini alikuwa Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids. Alibainisha kuwa imani ambayo kocha huyo ameionyesha kwake imekuwa chachu kubwa ya yeye kurejesha furaha na mapenzi yake kwenye mchezo wa soka.

Sababu za kuondoka Mamelodi Sundowns

Akiizungumzia klabu yake ya zamani, Mamelodi Sundowns, De Reuck alieleza kuwa idadi kubwa ya wachezaji klabuni hapo ilichangia yeye kukosa nafasi ya kucheza, jambo lililomlazimu kufanya maamuzi magumu ya kuondoka ili kuokoa kipaji chake.

"Sundowns ni klabu kubwa, lakini kuwa na kikosi cha wachezaji zaidi ya 40 kulifanya ushindani kuwa mkubwa sana na kupunguza nafasi ya kucheza mara kwa mara. Nilihitaji kwenda sehemu ambapo nitacheza na kuonyesha uwezo wangu, na ndio maana nilichagua Simba," alifafanua.

Mapenzi ya Mashabiki wa Simba

Licha ya hofu aliyokuwa nayo awali, De Reuck amesema ameshangazwa na mapokezi makubwa pamoja na upendo wa dhati anaopewa na mashabiki wa klabu hiyo tangu siku ya kwanza aliyokanyaga ardhi ya Tanzania.

"Sijawahi kuona mapenzi makubwa namna hii kwenye soka kama ninayoyapata kutoka kwa mashabiki wa Simba hapa nchini. Wamenifanya nijisikie nyumbani na wamenisaidia sana kusahau yaliyopita," alisema beki huyo kwa hisia.

Mbali na masuala ya soka, De Reuck aligusia pia maisha yake ya utotoni akieleza kuwa alikulia katika mazingira magumu na hatarishi huko Afrika Kusini, changamoto zilizomjenga kuwa imara hadi kufikia hatua aliyonayo sasa.

Kwa sasa, mchezaji huyo amekuwa mhimili muhimu katika safu ya ulinzi ya Simba SC, akionyesha kiwango thabiti kinachoendelea kuwateka mioyo mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi.

ADVERTISE HERE

Simba SC Stories

15 de Agosto yawasili Dar kwa mchezo dhidi ya Simba
15 de Agosto yawasili Dar kwa mchezo dhidi ya Simba
1h ago
READ MORE β†’
15 de Agosto wanaandaliwa dozi saizi yao
15 de Agosto wanaandaliwa dozi saizi yao
3h ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 20, 2026
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 20, 2026
5h ago
READ MORE β†’
CAF yabadili mwamuzi wa mchezo wa 15 de Agosto dhidi ya Simba SC
CAF yabadili mwamuzi wa mchezo wa 15 de Agosto dhidi ya Simba SC
19h ago
READ MORE β†’
Wanasimba kushuhudia mchezo dhidi ya 15 de Agosto kwenye skrini kubwa Mwembeyanga
Wanasimba kushuhudia mchezo dhidi ya 15 de Agosto kwenye skrini kubwa Mwembeyanga
23h ago
READ MORE β†’
Huyu Libasse ni moto kweli
Huyu Libasse ni moto kweli
1d ago
READ MORE β†’
Mnyama amepania kumaliza mechi mapema Jumatano
Mnyama amepania kumaliza mechi mapema Jumatano
1d ago
READ MORE β†’
Mara Paap!, Dube anatua Msimbazi
Mara Paap!, Dube anatua Msimbazi
1d ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Jumatatu, Oktoba 19 2026
Magazeti ya leo Jumatatu, Oktoba 19 2026
1d ago
READ MORE β†’
Barker aweka mkakati wa kuwaadhibu 15 de Agosto licha ya kuwazuia mashabiki
Barker aweka mkakati wa kuwaadhibu 15 de Agosto licha ya kuwazuia mashabiki
2d ago
READ MORE β†’