Katika ulimwengu wa soka, mara nyingi macho ya mashabiki huwa kwa washambuliaji wanaotikisa nyavu, viungo wanaotoa pasi za mwisho au wachezaji wanaowaburudisha watazamaji kwa mbwembwe zao.
Lakini ndani ya kikosi cha Simba SC, kuna mtu anayefanya kazi kubwa bila kelele nyingi. Ni beki wa kati Ismail Olivier Toure, ambaye taratibu amekuwa mmoja wa nguzo muhimu katika safu ya ulinzi ya Wekundu wa Msimbazi.
Raia huyo wa Ivory Coast alijiunga na Simba akitokea FC Baniyas ya Falme za Kiarabu (UAE), akiwa amekuja kuongeza nguvu katika eneo la ulinzi. Tangu kuwasili kwake, Touré ameendelea kuonyesha umahiri wake akiwa sehemu ya wachezaji muhimu katika safu ya ulinzi ya Sima.
Toure ni kitasa Simba
Tofauti na mabeki ambao huonekana zaidi kwa kufanya tackling kali au mapambano ya nguvu, Toure amekuwa akitumia zaidi uelewa wa mchezo na nafasi kuzuia hatari.
Anaonekana kuwa mchezaji anayependa kusoma hatua ya mshambuliaji kabla hajafanya uamuzi, jambo linalomsaidia kuzuia mashambulizi bila kulazimika kutumia nguvu nyingi.
Uwezo huo umemfanya kuwa sehemu muhimu ya mfumo wa Simba, hasa katika michezo ambayo timu inahitaji nidhamu kubwa ya kiulinzi.
Utulivu wenye mpira
Miongoni mwa vitu vinavyomtofautisha Toure ni namna anavyocheza akiwa na mpira miguuni.
Beki wa kisasa hatakiwi kuwa mzuri katika kuzuia pekee, bali pia anatakiwa kuwa na uwezo wa kuanzisha mashambulizi kutoka nyuma. Toure amekuwa akionyesha uwezo huo kwa kutulia anapopokea mpira na kutafuta njia sahihi ya kuwasogeza wenzake mbele.
Utulivu huo unawapa viungo nafasi ya kupanda na kuifanya Simba kuanza mashambulizi ikiwa na mpangilio badala ya kupiga mipira ya kubahatisha kutoka nyuma.
Hata mabao anafunga
Kama vile haitoshi kuwa ngome kwenye ulinzi, Toure ameanza pia kuonyesha tishio lake katika eneo la wapinzani.
Msimu huu ameanza vyema kwenye Ligi Kuu akiwa tayari amefunga mabao mawili, akionyesha umahiri wake katika kutumia mipira ya juu, hasa mipira ya adhabu na kona.
Hilo linaongeza thamani yake kwa Simba kwa sababu beki anayefanya kazi kubwa kulinda lango lake na wakati huo huo anaweza kwenda mbele na kufunga ni silaha muhimu kwa timu.
Licha ya kutozungumzwa sana, Toure ameonyesha hahitaji kuimbwa kila mara ili thamani yake ionekane. Kadiri anavyoendelea kuwa imara katika ulinzi na kuongeza mabao kwenye akaunti yake, ndivyo anavyozidi kuthibitisha kuwa Simba imepata beki ambaye anaweza kufanya kazi pande zote mbili za uwanja.