Baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam Fc ambao Simba waliupata dhidi ya Azam Fc, ushindi huo umepokelewa kwa shangwe kubwa na mashabiki wa Wekundu hao wa Msimbazi.
Matokeo hayo yaliifanya Simba iendeleze rekodi yake ya ushindi wa asilimia 100 msimu huu na zaidi kuchukua alama 3 dhidi ya timu ambayo katika misimu miwili imechangia kuvuruga hesabu za Simba kwenye mbio za ubingwa.
Msimu uliopita pekee, Simba ilichukua alama 1 tu dhidi ya Azam Fc baada ya matokeo ya suluhu ya bila kufungana dimba la Azam Complex huku ikifungwa mchezo mwingine.
Matokeo hayo unaweza kusema yalichangia Simba kukosa ubingwa kwa tofauti ya alama 2 dhidi ya watani zao Yanga.
Msimu huu uongozi wa Simba umekuja na mkakati wa kuhakikisha vikwazo vyote vilivyojitokeza msimu uliopita, vinafanyiwa kazi.
Kuna jitihada kubwa zinafanywa nje ya uwanja na viongozi wa Simba ikiwa ni pamoja na bonas kubwa ambayo wachezaji wanawekewa mezani kwenye kila mchezo.
Rais wa heshima wa Simba Bilionea Mohamed Dewji 'Mo' aliweka mezani Tsh Milioni 200 kwa wachezaji kushinda mchezo uliopita dhidi ya Azam Fc.
Lakini pia aliweka kitita kama hicho kwa Simba kufuzu hatua ya awali Ligi ya Mabingwa wakishinda mechi zote mbili dhidi ya Mighty Wonderers wakivuna Tsh Milioni 100 kwenye kila mchezo.
Baada ya ushindi dhidi ya Azam Fc sasa nguvu zote zinaelekezwa kwenye mchezo wa dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga ambao ndio unaofuata Oktoba 10 baada ya mapumziko ya kalenda ya FIFA.
Ni mchezo mwingine ambao Simba inahitaji kushinda ili kujisafishia njia ya ubingwa msimu huu. Ni wazi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa ni lazima kumfunga Yanga.
Mpaka sasa ingawa bado mapema, mbio za ubingwa zinaonekana kubaki kwa Yanga na Simba hivyo kuchukua alama tatu dhidi ya Yanga maana yake ni kujiweka hatua moja mbele.