Kocha Mkuu wa Simba Steve Barker amewapongeza wachezaji wake kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam Fc katika mchezo wa ligi kuu ya NBC uliopigwa uwanja wa Azam Complx Jumatano usiku.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Barker alisema walihitaji kuibuka na ushindi na jambo muhimu wameshinda bila ya kuruhusu bao.
Amesifu jinsi vijana wake walivyokuwa makini kwenye eneo la ulinzi wakiwanyima Azam Fc nafasi ya kulifikia lango huku wakitumia vyema nafasi za mashambulizi ya kujibu kuwaadhibu.
"Nimeridhishwa na jinzi tulivyoimarika katika ulinzi, tumekuwa na mpangilio mzuri kwenye ulinzi tukiwazuia wapinzani wetu kuliona lango letu."
"Leo tumeonyesha ubora katika kumiliki mpira na kujilinda, timu inayotaka kushambulia vizuri lazima pia iwe na uwezo wa kujilinda."
"Mchezo ulikuwa wa nguvu na kimbinu, nafikiri mwamuzi angeweza kuchukua hatua zaidi kwenye baadhi ya matukio lakini nimefurahi Simba kuondoka na ushindi bila kuruhusu bao," alisema Barker
Ushindi huo umeifanya Simba ifikishe alama 18 ikichuana na vikali na watani zao Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi timu zikitenganishwa na tofauti ya mabao ya kufunga.
Hata hivyo ushindi dhidi ya Azam Fc unaweza kusema ni alama tatu zenye thamani kubwa katika mkakati wa kutwaa ubingwa msimu huu.