Wekundu wa Msimbazi Simba SC, wameendelea kujiweka katika nafasi sahihi msimu huu baada ya kuichapa Azam FC mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Ushindi huo unaifanya Simba SC kuendeleza rekodi yao ya kutofungwa wala sare msimu huu, wakiendeleza rekodi ya asilimia 100 baada ya kushinda mechi sita mfululizo.
Chini ya benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Steve Barker, Wekundu wa Msimbazi wameonyesha soka safi na la kiwango cha juu wakidhihirisha dhamira yao ya dhati ya kurejesha umwamba wao kwenye soka la ndani.
Simba sasa imevuna alama 18 muhimu zilizoweka presha kubwa kwa wapinzani wao wa karibu.Kwa misimu ya karibuni, Azam FC imekuwa mwiba mchungu kwa Wekundu hao wa Msimbazi. Wanalambalamba hao wa Chamazi wamekuwa wakivuruga mara kwa mara hesabu za Simba katika mbio za ubingwa, jambo lililofanya mchezo wa leo kuwa zaidi ya mechi ya pointi tatu.
Idumba, Chama Waamua Mechi
Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa katika kipindi cha kwanza, uligeuka upande wa Simba katika kipindi cha pili. Lango la Azam FC lilifunguliwa kufuatia kosa la mlinzi wao, Nathaniel Idumba Fasika, aliyejifunga mwenyewe wakati akijaribu kuokoa hatari mpira uliopigwa kichwa na Rushine de Reuck.
Wakati Azam Fc wakijitahidi kurudi mchezoni, kiungo fundi raia wa Zambia, Clatous Chama, alipigilia msumari wa mwisho kwa kufunga bao la pili baada ya Simba kufanya shambulizi la kushitukiza na kuzima kabisa matumaini ya wenyeji na kuhakikishia Simba pointi tatu muhimu ugenini.
Simba ilionyesha kuwa hatari zaidi kwenye mashambulizi ya kujibu huku vijana wa Barker wakionyesha nidhamu ya hali ya juu katika ulinzi.

