Kiungo mshambuliaji wa Simba SC, Clatous Chama, ameonekana kutotikiswa na mijadala inayozunguka jina lake nje ya uwanja, akisisitiza kuwa mambo hayo hayana nafasi katika maisha yake ya soka.
Chama ameyasema hayo jana wakati wa tukio la Simba Media Day lililofanyika katika Uwanja wa MO Arena, Bunju jijini Dar es Salaam, huku kauli yake ikija wakati ambapo kumekuwa na mjadala mkubwa mitandaoni kuhusu uhusiano wake na klabu yake ya zamani, Yanga SC.
Nyota huyo wa Zambia amesema anachagua kuangalia zaidi kile kinachoendelea ndani ya uwanja na majukumu yake kama mchezaji wa Simba, badala ya kuruhusu mijadala ya nje ya uwanja kumvuruga.
"Mimi ni mchezaji mzoefu hayo masuala ya nje ya uwanja hayawezi kunisumbua, akili na mawazo yangu yako kwa klabu ya Simba ambayo mimi na wenzangu tunawajibika katika kuhakikisha tunfikia malengo," alisema Chama
Hivi karibuni Chama alifichua yaliyojiri wakati amesajiliwa na Yanga akiweka wazi kuwa haikuwa dhamira yake kujiunga na timu hiyo lakini mazingira ya wakati huo yalimfanya kuchukua uamuzi ambao ulimfanya asiwe na furaha.
Baada ya kurejea Simba, Chama amerejesha makali yake akiwa sehemu ya wachezaji wanaotegemewa katika kikosi cha Simba, huku mashabiki wakitarajia kuona ubora wake ukionekana zaidi ndani ya uwanja.