Unaweza kuwa na mashaka pale Simba inapocheza mechi za mashindano ya ndani, lakini jambo moja limekuwa likionekana wazi kwa miaka mingi, Mnyama anapokuwa kwenye michuano ya kimataifa, hubadilika kabisa.
Huu umekuwa kama utamaduni wa Simba SC. Kwa miaka mingi, Wekundu wa Msimbazi wamekuwa na kawaida ya kuvuka matarajio ya wengi wanaposhiriki mashindano ya CAF, iwe ni Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho.
Na jana, Simba imeendelea kuonyesha kwa nini inaheshimika kwenye jukwaa la kimataifa.
Ushindi muhimu licha ya kiwango kisichoridhisha
Simba ilifanikiwa kupata ushindi muhimu ugenini dhidi ya Mighty Wanderers, licha ya kutokuwa kwenye kiwango chake bora kwa muda mwingi wa mchezo.
Bao la Anicet Oura lilitosha kuwapa Wekundu wa Msimbazi ushindi ambao unaweza kuwa na thamani kubwa katika safari yao ya kutafuta tiketi ya hatua inayofuata.
Kilichovutia zaidi ni namna Simba ilivyoweza kupata matokeo katika mchezo ambao haikuonekana kucheza kwa kiwango cha juu.
Hii ndiyo Simba ambayo mashabiki wake wameizoea kwenye mashindano ya kimataifa, si lazima icheze vizuri kila dakika, lakini inajua namna ya kupata matokeo.
Ushindi huo umeiweka Simba katika nafasi nzuri kabla ya mchezo wa marudiano utakaopigwa Jumapili, Septemba 13.
Mnyama atahitaji ushindi au sare ili kuhakikisha inasonga mbele katika mashindano hayo.
Wengine chupuchupu Botswana, sare yashangiliwa
Wakati Simba ikiendeleza utamaduni wake wa kupata matokeo kwenye mashindano ya CAF, hali ilikuwa tofauti kwa watani zao, Yanga.
Yanga walionekana kuwa katika hatari ya kuondoka Botswana na kipigo, kabla ya kupata bao la kusawazisha dakika za lala salama.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ali, hakusita kuwapiga dongo watani zao baada ya matokeo hayo.
“Mnapata wapi nguvu ya kushangilia sare kwenye hatua hizi?” alihoji Ahmed.
Mnyama ameshinda ugenini, ameweka mguu mmoja katika hatua inayofuata na sasa anasubiri mchezo wa marudiano.