Klabu ya Simba SC imeanza vyema kampeni yake ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika (CAF Champions League) baada ya kupata ushindi muhimu wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Mighty Wanderers ya Malawi.
Mchezo huo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya awali ulipigwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Bingu, jijini Lilongwe, ambapo Wekundu wa Msimbazi walionyesha ukomavu mkubwa na kuondoka na mtaji mzuri wa goli la ugenini kuelekea mchezo wa marudiano.
Bao pekee na la ushindi katika mtanange huo lilipatikana kupitia kwa winga Anicet Oura.
Goli hilo lilikuja kufuatia mpango mkakati wa haraka, ambapo mlinda lango wa Simba, Djibrilla Kassali, alipiga mpira mrefu uliomkuta Oura ambaye hakufanya makosa kuwazidi ujanja mabeki wa Mighty Wanderers na kukwamisha mpira wavuni.
Baada ya goli hilo, wenyeji Mighty Wanderers walijaribu kushambulia kusaka bao la kusawazsha wakisukumwa na mashabiki wao wa nyumbani, lakini ngome ya ulinzi ya Simba na mlinda lango Kassali walikaa imara na kuzuia hatari zote hadi mwamuzi anapuliza filimbi ya mwisho.
Ushindi huu unaiweka Simba katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua inayofuata, kwani watakuwa wenyeji katika mchezo wa marudiano utakaopigwa jijini Dar es Salaam, ambapo watahitaji sare yoyote au ushindi ili kusonga mbele.