Wekundu wa Msimbazi, Simba SC, wako tayari kuanza safari yao ya kutafuta ubingwa wa Afrika watakapokutana na wenyeji Mighty Wanderers FC katika mchezo wa kwanza wa raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League).
Mchezo huo wa kusisimua umepangwa kuchezwa kesho Jumapili, Septemba 6, 2026, kwenye Uwanja wa Taifa wa Bingu, jijini Lilongwe, Malawi.
Mtanange huo unatarajiwa kuanza majira ya saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, huku mashabiki wakitarajiwa kushuhudia pambano hilo mubashara kupitia Azam Sports 2 HD.
Simba yawasili Malawi ikiwa na morali kubwa
Simba imewasili nchini Malawi ikiwa na morali kubwa baada ya kuanza vyema msimu wa Ligi Kuu ya NBC, ambapo Wekundu hao wa Msimbazi wameshinda michezo yao yote mitano ya mwanzo.
Kikosi hicho kinachoongozwa na kocha Steve Barker kimewasili kikiwa na nyota wake wote, wakiwemo Clatous Chama, Elie Mpanzu, Libasse Gueye, Anicet Oura na kiungo fundi Ibrahim Jabeer, huku matarajio yakiwa ni kuondoka Malawi na matokeo mazuri kabla ya mchezo wa marudiano jijini Dar es Salaam.
Barker amesisitiza kuwa Simba haiendi Malawi kwa ajili ya kumdharau mpinzani, bali inahitaji kucheza kwa umakini na nidhamu ili kupata matokeo yatakayoiweka kwenye nafasi nzuri kuelekea mchezo wa pili.
Mighty Wanderers wanaingia na faida ya nyumbani
Kwa upande wa wenyeji, Mighty Wanderers wanaamini kuwa kucheza mbele ya mashabiki wao kutakuwa silaha muhimu katika pambano hilo.
Timu hiyo imeonyesha kiwango kizuri kwenye Ligi Kuu ya Malawi, ambapo katika michezo 15 imefanikiwa kushinda mara nane na kupoteza mchezo mmoja pekee.
Hatari kubwa kwa Simba inatajwa kuwa kwenye safu yao ya ushambuliaji, inayowaamini Promise Kamwendo na Lameck Mithi. Washambuliaji hao tayari wamefunga mabao matano kila mmoja kwenye ligi, hivyo safu ya ulinzi ya Simba itapaswa kuwa makini kwa dakika zote 90.
Mighty Wanderers pia inaongozwa na kocha Patrick Mabedi, ambaye ana uzoefu wa soka la Tanzania, jambo linaloweza kumpa uelewa wa ziada kuhusu aina ya mchezo wa Simba.
Wanderers pia wana ulinzi imara
Mchezo huu pia utakuwa mtihani mkubwa kwa safu ya ushambuliaji ya Simba. Mighty Wanderers wameonyesha uimara mkubwa katika ulinzi kwenye mechi zao za ligi, wakiruhusu mabao tisa pekee katika michezo 15.
Hivyo, Simba italazimika kutumia ubunifu mkubwa kuvunja ngome hiyo, huku macho yakielekezwa kwa washambuliaji wake wakiongozwa na Gueye ambaye unaweza kusema kwa sasa ndio anabeba kufungua za milango ya wapinzani kwani katika mechi tano za ligi kwenye ligi amehusika kwenye mabao sita akifunga 1 na kutoa pasi 5.
Uzoefu wa Simba Afrika wawaongezea mzigo Wanderers
Licha ya Mighty Wanderers kuwa na faida ya uwanja wa nyumbani, Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na uzoefu mkubwa zaidi katika mashindano ya klabu barani Afrika.
Wekundu wa Msimbazi wamekuwa washiriki wa mara kwa mara kwenye michuano ya CAF, ikiwa ni pamoja na kufika hatua za juu za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Uzoefu huo unaweza kuwa muhimu katika mchezo wa aina hii, hasa katika kukabiliana na presha, mazingira ya ugenini na umuhimu wa kupata matokeo kabla ya mchezo wa marudiano.
Mwamuzi Kutoka Ghana
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limemteua Charles Bulu kutoka Ghana kuwa mwamuzi wa kati wa mchezo huo. Bulu atasaidiwa na waamuzi wengine kutoka Ghana na Nigeria.
Mchezo wa marudiano Dar es Salaam
Baada ya mchezo wa Jumapili nchini Malawi, Simba na Mighty Wanderers watakutana tena kwenye mchezo wa marudiano Septemba 13, 2026, jijini Dar es Salaam.
Hapo ndipo mshindi wa jumla atapatikana na kupata nafasi ya kusonga mbele kwenye raundi inayofuata ya mashindano hayo.
Mshindi wa jumla katika mikondo hiyo miwili atakutana na mshindi kati ya 15 de Agosto ya Equatorial Guinea na Fomboni FC ya Comoro.
Ni Siku ya Simba Kuunguruma
Kwa Simba, safari ya kutafuta mafanikio katika msimu mpya wa mashindano ya Afrika inaanza Malawi.
Wekundu wa Msimbazi wanaingia uwanjani wakijua wazi kuwa ushindi ugenini unaweza kuwa hatua kubwa kuelekea kufuzu, lakini Mighty Wanderers nao wana ndoto zao mbele ya mashabiki wao.
Dakika 90 za Lilongwe zitatoa jibu la kwanza huku Simba ikiwa na faida ya kumaliza mchezo wa pili uwanja wa nyumbani.