Aussems awatahadharisha wapinzani wake

Mwana Msimbazi By Mwana Msimbazi
•
2 Aug 2018
Aussems awatahadharisha wapinzani wake
Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussemms ndio kwanza ana wiki mbili tu tangu aliposaini mkataba wa kukinoa kikosi cha mabingwa hao wa soka nchini na hakuwahi kufanyiwa mahojiano, kwani aliposaini tu alipaa zake Uturuki.

Katika mahojiano yake ya kwanza na gazeti la Mwanaspoti, Aussemms ameweka bayana mipango kamambe aliyotua nayo nchini ili kuipaisha Simba, lakini akisisitiza anapenda soka la ushindani ili hata kama timu yake ikifungwa ama kushinda basi matokeo yawe ni ya kutokwa jasho kwelikweli.

Pia amefichua anatambua wapinzani wakubwa wa Simba ni Yanga na hata Azam na angependa kuona anakutana na timu hizo zikiwa kamili ili kuipa changamoto timu yake, sambamba na kuanikia falsafa na misimamo yake kama kocha. Endelea..

NI MTU MAKINI

Kocha Patrick Winand Ausemms aliyezaliwa Feb 6, 1965 mjini Moelingen, Ubelgiji ni pande la mtu kwelikweli, ni baba wa miraba minne aliyekata hewa akiwa na urefu wa futi 6 na inchi 3 ana mwili wa mazoezi haswa na sio manyama uzembe.

Kidevuni amefuga ndevu katika mtindo maarufu kwa vijana wa mjini kama mzuzu na kichwani ana kipara cha kiaina maarufu kama ‘unga’.

Achana na mwonekano wake, tabia ya huyu jamaa ni mtu makini, mtulivu na anatumia zaidi akili katika maamuzi yake si mtu wa papara.

Si mwongeaji sana, ni mtu wa vitendo na hata anapokuwa na wachezaji wake uwanjani, mazungumzo kidogo lakini vitendo na kazi ni zaidi.

Hata baadhi ya wachezaji wamemwelezea Aussems kama mmoja wa makocha wa aina yake ambaye anawafanya wajisikie raha kufundishwa naye na kumuelewa kwa sababu anawanoa kwa vitendo kama afanyavyo Masoud Djuma.

AITEGA YANGA

Ausemms ambaye katika enzi zake za uchezaji alikuwa anacheza nafasi ya beki anasema, anajua Simba ni timu kubwa, lakini kwa wadau wa soka, wanachama wa Simba pamoja na mashabiki wote atawapa zawadi ya kuona mpira safi wa pasi za kideoni huku akiwataka wapinzani wao kama Yanga, Azam na wengine waonyeshe.

“Napenda kucheza ligi yenye ushindani na isiwe timu moja tu ndio inashinda na nyingine zinafanya vibaya,” anasema Ausemms aliyestaafia soka katika klabu ya Troyes AC ya Ufaransa mwaka 1993.

“Najua wapinzani wakubwa wa Simba ni Yanga siku zote na hizo nyingine ikiwemo Azam zinafuata, tutakapokuwa kwenye ligi, upinzani uonekane kweli ndiyo inakuwa vizuri.

Nataka Simba ikutane na timu zilizokamilika na kutoa upinzani.”

Anasema, anaamini Yanga, Azam na wengine wakiwa bora, Simba itakuwa bora zaidi kwa sababu kile anachowafunza wachezaji wake watakidhihirisha kwa mafanikio na kuifanya timu itishe zaidi.

Mbelgiji anasema ili timu iwe bora lazima wanaokufuata nao wawe bora lakini kama ligi ya ubora wa upande mmoja na wengine wanafanya vibaya inachangia kuifanya ligi iwe dhaifu na kutoa matokeo yasiyo na uwiano sawa.

Na ikifika wakati ambao timu hizo pinzani zinakutana ndio ubabe wao uonekane na timu mojawapo ikifungwa ionekane kweli ilikuwa mechi ya ‘derby’ kwelikweli.

Lakini wakati Ausemms anazungumza ushindani huo wapinzani wa Simba, yaani Yanga, haina matokeo mazuri tangu mwishoni mwa msimu uliopita kwani ilimaliza Ligi Kuu ikiwa pungufu ya alama 17 dhidi ya mabingwa Simba.

Simba alibeba taji ikiwa na alama 69, ikifuatiwa na Azam walikuwa na pointi 58 na Yanga ikiwa ya tatu na alama zao 52, kila moja ikicheza mechi 30 za msimu mzima.

FALSAFA YAKE KISOKA

Ausemms, aliyewahi kuwanoa Mabingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika 2012, AC Leopards ya Congo kwa mafanikio anafafanua falsafa yake kubwa ya mafanikio ni kuzingatia muda.

“Ninapenda muda. Katika maisha huwezi kupata mafanikio ndani ya kipindi kifupi, mipango na muda ndiyo kila kitu,” anasema.

“Kitu chochote kizuri kinahitaji maandalizi na muda na ndicho ninachokiamini.”

Lakini pia anasema kisoka anapenda na kuhitaji timu yake icheze soka la kitabuni yaani kampa...kampa tena.

Anasema, soka analohitaji ni mpira wa kucheza na si kubutua ilimradi kupata matokeo kwa sababu anajua mashabiki wanaenda uwanjani kufuata burudani, hivyo lazima lazima watu wafurahie ufundi.

“Unapocheza soka la kubutua ni ngumu kupata matokeo mazuri nataka mpira uchezwe kuanzia nyuma kwa kipa na mabeki na uendelee mbele kwa viungo na washambuliaji na si kupiga tu unabutua,” anafafanua.

“Mpira uchezwe kwa pasi fupi na ndefu bila kupoteza muda, unapiga moja, mbili unaachia ndiyo mpira wa kisasa soka la kuvutia, timu ikicheza hivi kocha unafurahi na hata mashabiki watakuwa na furaha pia.”

Anasema, kwa kawaida mbali na matokeo, mashabiki wanataka raha waone ushindi umetokana na kitu gani na si ilimradi mmeshinda.

UKUTA WA CHUMA

Ausemms anasisitiza kuwa, katika mbinu zake za ushindi timu yake inapocheza lazima iwe na mabeki wanne nyuma yaani mfumo wowote lazima uanze na 4 zinazofuata huko yeye hata hajali.

“Mfumo unategemea na aina ya wachezaji utakaokua nao kwenye timu, lakini pamoja na yote mimi napendelea zaidi timu yangu inapocheza iwe na mabeki wanne nyuma na si vingine,” anasema.

“Unapokuwa na mabeki wanne nyuma ni ulinzi tosha na unatoa nafasi kubwa ushindi. Ninapokuwa na mabeki hao, wachezaji wanaocheza mbele sijali wakataa katika mfumo wowote kulingana na timu pinzani inavyocheza.

“Inaweza kuwa mfumo wa 4-3-3 ama 4-4-2 au 4-5-1 ilimradi tu timu nyuma iwe na mabeki wanne, hii inasaidia pia kuifanya timu kuwa na ukuta mgumu kupitika.”

Kutokana na hilo, iko wazi kuwa mfumo ule wa awali uliokuwa ukitumika Simba wa mabeki watatu nyuma umekufa. Awali Simba ilikuwa ikitumia zaidi mfumo 3-5-2 na huu ulikuwa ukitumiwa zaidi na kocha msadizi wa sasa Mrundi Masoud Djuma.

MECHI TATU TU KWAKE FRESHI

Ausemms anasema, anataka kikosi chake kicheze mechi tatu za kirafiki na mchezo wa kwanza ulianza jana Jumatano dhidi ya Mouloudia Oujda FC ya Morocco.

“Katika mechi hizo ndio nitajua timu yangu vizuri ni ipi nitakayoanza nayo kikosi cha kwanza, kwa sasa tunacheza tu na kuangalia mchezaji mmoja mmoja na mwisho wa siku mambo yatakuwa safi,” anasema.

“Wapo wachezaji wanajulikana kwa kufanya vizuri na baadhi nimewaona katika mechi za Kagame Cup lakini si kwamba nawajua, nataka wanionyeshe sasa katika mazoezi tunayofanya na mechi tutakazocheza huku Uturuki,” anasema.

Kocha Aussems anasema, anachohitaji ni mchezaji mwenye utayari na hamu ya kufanya kazi yeye mwenyewe bila kushurutishwa.

Ausemms anasema, kambi waliyoweka Uturuki ni ya kisasa wanapata kila kitu, vifaa vya michezo kwa mahitaji yao, malazi pamoja na hali ya hewa.

“Tuko vizuri kabisa kila kitu kinakwenda sawa hii ndiyo kambi tunayoihitaji kwa sababu kila tunachokihitaji kipo,” anasema.

“Tuna kila kitu tunachokitaka, vifaa vyote vya mazoezi, viwanja vizuri vya mazoezi, mazingira na hali ya hewa nzuri, malazi mazuri yaani kila kitu, ninafuraha na wachezaji pia wana furaha.”

Katika hoteli ambayo Simba wamefikia, imejitenga kabisa na mji ambako kuna watu mchanganyiko na pilika za hapa na pale. Yenyewe ipo juu mlimani na imezungukwa na milima na misitu mikubwa na kutoka hapo mpaka kwenye makazi hayo mchanganyiko ya watu yaani Kartepe mjini, unatumia zaidi ya dakika 20.

AKUNWA NA VIPAJI

Katika kipindi cha maandalizi, kocha amekuwa akiangalia vipaji vya kila mchezaji, tabia na mbinu za kwenda nao sawa ili wamfanyie kazi yake vizuri na anasema. “Mpaka sasa tumefanya mazoezi kwa vipindi 16 nimeona wachezaji wanafuata kila ninachowafundisha kwangu ni furaha,” anaeleza na kufafanua zaidi;

“Nina wachezaji wenye vipaji ambavyo kama wataendana na kile ninachofundisha na kukihitaji sina wasiwasi kabisa na kazi yangu naamini vijana hawataniangusha.”

Aussems anasema kujaa kwa vipaji kikosini kunamrahisishia kazi katika kuwalisha wachezaji hao mbinu na ufundi wake, ili kuisaidia timu na anaamini mpaka watakaporudi nchini kujiandaa na msimu mpya wa ligi vijana wake wataiva vyema.

NIDHAMU KWANZA

Ausemms anasema, amekaa chini na wachezaji wake na kuzungumza mambo mengi, kitu cha kwanza ili kazi yao ifanikiwe muda wa kufanya kazi ni kazi, lakini wakati wa kufurahi ni kufurahi.

Anasema, yeye ni muumini mzuri wa nidhamu na anachoamini, kwa mchezaji mwenye nidhamu kazi itakuwa nzuri.

Anatolea mfano katika mazoezi yake yanayoendelea Uturuki wachezaji wamekuwa wakifanya hivyo na inamwonyesha wanazingatia kile anachofundisha.

Mahojiano haya ni kwa hisani ya gazeti la Mwanaspoti
ADVERTISE HERE

Simba SC Stories

Janza atangazwa Mkurugenzi wa ufundi Simba
Janza atangazwa Mkurugenzi wa ufundi Simba
2h ago
READ MORE →
Barker hamuhofii yeyote makundi CAFCL
Barker hamuhofii yeyote makundi CAFCL
4h ago
READ MORE →
Fountain Gate wanaandaliwa dozi inayowatosha
Fountain Gate wanaandaliwa dozi inayowatosha
5h ago
READ MORE →
Mkutano Mkuu Simba sasa ni Januari 2027
Mkutano Mkuu Simba sasa ni Januari 2027
7h ago
READ MORE →
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
12h ago
READ MORE →
Mechi dhidi ya Fountain Gate yasogezwa mbele kwa siku moja
Mechi dhidi ya Fountain Gate yasogezwa mbele kwa siku moja
23h ago
READ MORE →
Simba kumuongeza Barker mkataba wa muda mrefu
Simba kumuongeza Barker mkataba wa muda mrefu
1d ago
READ MORE →
Simba yaifuata Fountain Gate Manyara
Simba yaifuata Fountain Gate Manyara
1d ago
READ MORE →
Hii hapa miamba 16 makundi CAFCL
Hii hapa miamba 16 makundi CAFCL
1d ago
READ MORE →
Highlights; Simba 3-0 15 de Agosto, CAFCL (FT)
Highlights; Simba 3-0 15 de Agosto, CAFCL (FT)
1d ago
READ MORE →