Mbelgiji akubali kuinoa Simba

Mwana Msimbazi By Mwana Msimbazi
•
10 Jul 2018
Mbelgiji akubali kuinoa Simba
Simba kesho Jumatano itashuka Uwanja wa Taifa katika nusu fainali ya Kombe la Kagame dhidi ya JKU, lakini habari njema kwa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi ni taarifa za Kocha Mbelgiji Patrick Aussems kuamua kukubali kufanya kazi Msimbazi.

Awali kocha huyo alitua Jumapili ya wiki iliyopita na kufanya mazungumzo na mabosi wa Simba chini ya Bilionea Mohammed ‘MO’ Dewji kabla ya kuamua kurudi kwao ili kwenda kutafakari ofa aliyokuwa amepewa na inaelezwa kuwa ameafiki kazi.

Inaelezwa kabla ya kuondoka, Mbelgiji huyo na Simba walikubaliana kila mmoja aende akatafakari madau waliyowekeana mezani baada ya kutokea mvutano na ndipo akiwa kwao kocha huyo amewapigia mabosi wa Simba kuwaambia yupo tayari kurudi nchini.

Jambo hilo limewafanya Simba kufurahia na kumtaka awasili Julai 17 na siku chache baadaye atimke na timu kuelekea Uturuki kwa ajili ya kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na michuano mingine ambayo Simba itashiriki.

Habari kutoka kwa mmoja wa vigogo wa Simba, zinasema kuwa Aussems aliyewahi kuwanoa mabingwa wa zamani wa Kombe la Shirikisho Afrika, AC Leopards ya Congo Brazzaville, amekubali kurudi kusaini mkataba wa mwaka mmoja waliokubaliana katika mazungumzo yao.

MSHAHARA WAKE

Alidokeza kuwa kocha huyo atavuta mshahara wa dola 10,000 ambao ni zaidi ya Sh22 milioni, ambaop ni nusu ya fedha alizokuwa akilipwa Mfaransa Pierre Lechantre aliyetimka klabuni hapo mara mkataba wake wa miezi sita ulipomalizika.

“Mshahara atakaolipwa hautazidi dola 10,000 na kubwa ni kwamba ni kocha asiye na gharama kubwa, ni tofauti na alivyokuwa Lechantre ambaye safari zake zote nchini alikuwa akisafiri kwa ndege, huku akivuta zaidi ya mshahara wa Aussems,” kigogo huyo aliyeomba kuhifadhiwa jina alisema.

“Patrick pia ameomba kubakishiwa benchi la ufundi kama lilivyo sasa na amesisitiza hatapenda kufanya kazi na Kocha Msaidizi ambaye atakuwa anakubali kila analoambiwa, bali kasema atamtaka yule atakayekuwa akimpa changamoto,” aliongezea kigogo huyo.

KAMBI YA UTURUKI

Inaelezwa kuwa Kocha huyo anatarajiwa kutua mapema kabla ya Simba kuanza safari ya kuelekea Uturuki kuweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa mashindano.

Inaelezwa kambi hiyo huenda ikatumia zaidi ya fedha zilizotumika katika kambi ya msimu uliopita iliyowekwa Afrika Kusini ambayo ilitumia Sh120 milioni na kwamba safari hiyo itakuwa kati ya Julai 19 na 20.

“Tulienda Afrika Kusini tulitumia Sh120 milioni, hivyo hiyo ya Uturuki huenda isiwe chini ya Sh250 milioni ambayo tutatumia katika safari yote na kila kitu,” alisema kiongozi huyo ambaye atakuwa na jukumu la kuratibu safari hiyo ya Uturuki.

Kuhusu kambi hiyo, Meneja wa Simba, Richard Robert ‘Mwana’ alisema wanachoangalia kuhusu kambi ni utulivu na umakini wa mahala ambapo watakwenda kuweka kambi tena kulingana na benchi la ufundi linavyotaka.

“Mipango yote inakwenda vizuri na baada ya kumaliza Kagame tutasafiri na kikosi kizima hadi wale waliokuwa mapumziko,” alisema Mwana.

Naye Mratibu wa Simba Abbas Selemani, alisema mchakato na mipango ya kwenda Uturuki inakwenda sawa na tayari wameshaanza kushuhgulikia viza kwa wachezaji, benchi la ufundi wa wachezaji wote watakao kwenda.

“Ubalozi wa Uturuki na Tanzania kuna urafiki na ukaribu kati yetu kwahiyo haitakuwa shida kwetu kusafiri hata gharama na imani hazitakuwa juu sana na hesabu kamili ya tulichotumia nitakuwa nayo baada ya kurudi nchini,” alisema Abbas.

MKONGO ATESTI MITAMBO SIMBA

Kiungo Mkongo Kakule Mugheni Fabrice aliyekuwa uwanjani juzi Jumapili akishuhudia Simba ikishinda kwa mbinde dhidi ya AS Port, ameanza tizi huku Kocha Masoud Djuma akisema hajaja kufanya majaribio, bali kusajiliwa kabisa.

Amesema anamjua kiungo huyo na aliwahi kumnoa Kiyovu Sports ya Rwanda kwa miaka miwili, hivyo ana uhakika na kiwango chake.

“Huyu si mchezaji wa kufanyiwa majaribio, bali amekuja ili kusajiliwa Simba, japo inategemea na maamuzi ya mabosi, kama kocha naufahamu uwezo wake,” alisema Mrundi huyo.

Mwanaspoti
ADVERTISE HERE

Simba SC Stories

Magazeti ya leo Jumatano, Oktoba 28 2026
Magazeti ya leo Jumatano, Oktoba 28 2026
2h ago
READ MORE →
Janza atangazwa Mkurugenzi wa ufundi Simba
Janza atangazwa Mkurugenzi wa ufundi Simba
16h ago
READ MORE →
Barker hamuhofii yeyote makundi CAFCL
Barker hamuhofii yeyote makundi CAFCL
19h ago
READ MORE →
Fountain Gate wanaandaliwa dozi inayowatosha
Fountain Gate wanaandaliwa dozi inayowatosha
20h ago
READ MORE →
Mkutano Mkuu Simba sasa ni Januari 2027
Mkutano Mkuu Simba sasa ni Januari 2027
22h ago
READ MORE →
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
Magazeti ya leo Jumanne, Oktoba 27 2026
1d ago
READ MORE →
Mechi dhidi ya Fountain Gate yasogezwa mbele kwa siku moja
Mechi dhidi ya Fountain Gate yasogezwa mbele kwa siku moja
1d ago
READ MORE →
Simba kumuongeza Barker mkataba wa muda mrefu
Simba kumuongeza Barker mkataba wa muda mrefu
1d ago
READ MORE →
Simba yaifuata Fountain Gate Manyara
Simba yaifuata Fountain Gate Manyara
1d ago
READ MORE →
Hii hapa miamba 16 makundi CAFCL
Hii hapa miamba 16 makundi CAFCL
2d ago
READ MORE →